Helb motoni kwa kukiuka masharti ya riba ya mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) imejikuta katikati ya mzozo unaozidi kupanuka kuhusu riba na adhabu za mikopo ambazo, kwa miaka mingi, zimekuwa zikiongezeka hadi kuzidi mno kiasi kilichokopwa na wanafunzi.
Haya yanajiri baada ya Mahakama Kuu kutangaza kwamba bodi hiyo inapaswa kuzingatia kanuni ya sheria inayokataza riba kuzidi kiwango cha mkopo wa awali.
Uamuzi huo sasa umechochea wito mpya wa kufungua kesi ya pamoja kutoka kwa maelfu ya wahitimu waliokumbwa na mzigo wa madeni.
Kanuni inayofahamika kama In-duplum, neno la Kilatini lenye maana ya ‘mara mbili,’ inaeleza kuwa riba inapaswa kusimama mara tu inapofika kiwango sawa na mkopo uliochukuliwa.
Uamuzi huo umesababisha HELB kujitetea na kusisitiza kuwa imekuwa ikifuata sheria hiyo ya in-duplum, kufuatia malalamishi ya umma kuhusu ongezeko la madeni.
“Hii ina maana kuwa akaunti zote za HELB zinaendeshwa kwa mujibu wa uamuzi huu. HELB itaendelea kusimamia mikopo kwa haki, kisheria na kwa uwazi,” bodi hiyo ilisema.
Katika hukumu iliyotolewa Nairobi mnamo Agosti 2022, mahakama ilishikilia kwamba HELB, kama benki na wakopeshaji wengine, lazima itii kanuni ya in-duplum, licha ya madai yake kwamba inafanya kazi chini ya sheria maalumu.
Kesi hiyo ililetwa na wahitimu watatu wa vyuo vikuu waliodai kuwa HELB imekuwa ikiweka riba na adhabu “zisizostahimili” zilizofanya madeni yao kuzidi mara mbili kiwango walichokopa.
Jaji alikubaliana na hoja zao, akitaja mfumo huo kuwa wa kibaguzi na kinyume cha Katiba.
“Kwa lugha rahisi, kanuni hii inamaanisha riba inapaswa kusimama ikifikia kiwango cha mkopo,” jaji alisema, akiongeza kuwa Bunge liliidhinisha sheria hiyo “kuwazuia wakopeshaji waliogeuza riba kuwa biashara ya kujipatia fedha.”
Kwa miaka mingi, wahitimu wengi wamelalamikia riba na adhabu zinazoongezeka kwa kasi kiasi kwamba, wakichelewa tu kulipa, wanajikuta katika mzigo usioweza kulipika.
Mmoja wa walalamishi, kijana mwenye ulemavu aliyekopa Sh82,980 mwaka 2004, alijikuta akidaiwa Sh540,464 mwaka 2016 licha ya riba ya asilimia mbili pekee. Wengine wawili waliokopa takriban Sh140,000 mwaka 2016, walijikuta na madeni ya zaidi ya Sh335,000 mwaka 2021.
Mahakama ilitaja takwimu hizo kuwa “zinazokosa busara,” zikionyesha jinsi zilivyofikia mara mbili ya mkopo kwa muda mfupi.
HELB ilitetea adhabu zake, ikisema faini, ikiwemo Sh5,000 kwa kila mwezi wa kuchelewa, zimewekwa kisheria. Bodi ilidai tayari imekuwa ikipunguza riba kufikia kiwango cha mkopo tangu ilipopokea malalamishi, hata kabla ya kesi.
Lakini mahakama ilikataa hoja hiyo, ikisema wanafunzi hawapaswi kukabiliwa na masharti magumu kuliko wakopaji benki, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wanatoka katika familia maskini.
Uamuzi huo ulisisitiza kuwa riba na faini zinazozidi mkopo zinakiuka haki za kijamii chini ya Ibara ya 43 ya Katiba na haki za watumiaji chini ya Ibara ya 46.