Makala

Shirika laonya mvua kubwa itanyesha Kenya kwa miezi mitatu

Na BENSON MATHEKA January 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Kenya ni miongoni mwa nchi zitakazopokea mvua nyingi kuliko kawaida katika miezi ya Machi, Aprili na Mei, Mamlaka ya Maendeleo ya Nchi za Upembe wa Afrika (IGAD) imeonya.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Januari 27, IGAD ilisema kuna uwezekano wa asilimia 45 kwamba maeneo ya Kati na Magharibi mwa Kenya yatashuhudia mvua kubwa, sambamba na mataifa mengine ya Afrika Mashariki yakiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania, Djibouti na Somalia.

“Kuna uwezekano wa asilimia 40 wa mvua za karibu na wastani katika maeneo ya magharibi na mashariki mwa Sudan Kusini, kaskazini-mashariki na kusini-magharibi mwa Kenya, sehemu kubwa za Somalia, pwani ya Tanzania na maeneo machache ya Uganda na Ethiopia,” IGAD ilisema.

IGAD iliongeza kuwa mvua inatarajiwa kuanza kwa wakati wa kawaida au mapema katika sehemu nyingi za eneo hili, huku baadhi ya maeneo ya Ethiopia, Sudan Kusini na Somalia yakitarajiwa kushuhudia kuchelewa kwa kuanza kwa mvua.

Hata hivyo, shirika hilo lilibainisha kuwa baadhi ya maeneo, yakiwemo sehemu za pwani ya Kenya, yatashuhudia hali ya ukame zaidi ya kawaida katika kipindi hicho.

Zaidi ya hayo, IGAD ilisema baadhi ya maeneo ya Kenya, Sudan, Djibouti, Ethiopia na Tanzania yanaweza kushuhudia viwango vya joto vilivyo juu ya wastani katika kipindi hicho.

“Licha ya mtazamo wa msimu, vipindi vya ukame bado vinaweza kutokea katika maeneo yanayotabiriwa kupokea mvua za karibu au zaidi ya wastani, na vipindi vya mvua vinaweza kutokea katika maeneo yanayotabiriwa kupokea mvua za karibu au chini ya wastani,” IGAD ilisema.

Tangu mwanzo wa Januari, Kenya imekuwa ikishuhudia hali ya jua kali na ukame, hali inayotarajiwa kuendelea hadi mwisho wa Februari.

Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya ilisema sehemu kubwa ya nchi itasalia kavu kwa ujumla, huku mvua nyepesi pekee zikitarajiwa kati ya Jumanne, Januari 27, na Jumamosi, Januari 31.

Kwa mujibu wa utabiri huo, wakazi wa kaunti za Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi watashuhudia hali ya jua na ukame katika sehemu kubwa ya wiki, huku viwango vya juu vya joto vikifikia hadi nyuzi joto 30 za Selsiasi.

Hali kama hiyo inatarajiwa kushuhudiwa katika kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado na Taita Taveta, pamoja na maeneo ya ndani ya Kaunti ya Tana River na kaunti za ukanda wa pwani.

“Hali ya hewa ya jua na ukame inatarajiwa kutawala sehemu kubwa ya nchi; hata hivyo, mvua za hapa na pale zinaweza kushuhudiwa katika maeneo machache, hasa Nyanda za Juu mashariki na magharibi mwa Bonde la Ufa, eneo la Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria na nyanda za chini za kusini-mashariki,” idara hiyo ilisema.