Familia 83,000 zanufaika kupitia mradi wa ufugaji
Zaidi ya familia 83,000 katika kaunti 10 zinanufaika kupitia mradi wa uimarishaji ufugaji, miundombinu ya maji na masoko yaliyoboreshwa, unaolenga kugeuza ufugaji kuwa biashara yenye faida.
Kenya Livestock Commercialization Project (KeLCoP), ni mradi unaofadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Kenya, Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na wadauhusika, ukilenga kusaidia wafugaji wakiwemo wale wa kuhamahama ili kuongeza uzalishaji, kupanua vyanzo vya mapato na kujenga biashara zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo unatarajiwa kupata ufadhili zaidi wa Dola milioni 54.776 (sawa na Ksh7.12 bilioni), pamoja na kuongezewa muda wa miaka minne ili kupanua uwekezaji katika mifugo, uzalishaji unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, biashara zinazoendeshwa na vijana na uendelezaji wa masoko.
Ufadhili huo wa ziada na kuongezwa kwa muda wa mradi kunafuatia ziara ya pamoja kutathmini utendakazi wake iliyoongozwa na Mkurugenzi wa IFAD nchini Kenya, Matteo Marchisio. Kikos cha afisa huyo kilikagua maendeleo ya mradi, kutathmini mafanikio yake na kubaini maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika awamu inayofuata.
Walizuru kaunti za Siaya, Busia, Bungoma, Kakamega, Baringo na Nakuru, ambako mradi huo unasaidia jamii kukabiliana na changamoto za uhaba wa maji, gharama kubwa za uzalishaji na ukosefu wa masoko bora na ya kutegemewa.
“Mradi huu unasaidia jamii kuachana na ufugaji wa kujikimu pekee kwa kuwekeza katika miundombinu bora, kuzipa ujuzi na kuwaunganisha na masoko yenye ushindani mkuu,” alisema Bw Marchisio.
Alieleza kuwa mojawapo ya hatua muhimu ni kujenga miundombinu ya maji, ikiwemo visima virefu na mabwawa ya kuvuna maji. Hatua hiyo inapunguza muda ambao familia hutumia kutafuta maji, huku ikiboresha afya ya mifugo na kusaidia shughuli nyingine za kilimo.
Aliongeza kuwa upatikanaji wa maji umewezesha jamii nyingi kujihusisha na kilimo cha mboga, uzalishaji wa malisho ya mifugo na ufugaji wa nyuki, hivyo kuongeza mapato na kupunguza utegemeaji wa mifugo pekee.

Ili kuhakikisha miundombinu hiyo inadumu, jamii zimeunda kamati za usimamizi zinazokusanya ada ndogo kutoka kwa watumiaji ili kugharamia ukarabati, huku zikitoa nafasi za ajira kwa wenyeji.
Upandaji miti karibu na vyanzo muhimu vya maji wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mazingira mwaka huu pia uliimarisha juhudi za kuhifadhi mazingira na kulinda raslimali za maji. Kenya huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mazingira mnamo Oktoba kila mwaka, uhifadhi wa mazingira ukihamasishwa na kufuatwa na kampeni ya kitaifa ya upanzi wa miti.
Masoko na mifugo bora
Kenya Livestock Commercialization Project inawekeza kwenye masoko ya mifugo, uchinjaji, maghala ya kuhifadhi nyasi na vituo vya kuongeza thamani ya bidhaa ili kuboresha biashara na kuimarisha uhusiano kati ya wafugaji na wanunuzi.
Marchisio alisema usimamizi bora wa masoko ya mifugo unasaidia kupunguza wizi, kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kuweka taratibu wazi za biashara. “Baadhi ya vituo vya kuchinja vimeanza kutumika, huku vingine vikikaribia kukamilika kabla ya kukabidhiwa kwa vyama vya ushirika vya wenyeji na kamati za usimamizi,” alidokeza afisa huyo.
Serikali za kaunti pia zinatayarisha sheria za kudhibiti masoko ya mifugo ili kuboresha usimamizi na kuhakikisha miundombinu hiyo inadumu.
Kulingana na Bw Marchisio, ufugaji wa kuku wa kienyeji unaimarika, huku baadhi ya vikundi vikiongeza idadi ya kuku kutoka wachache hadi mamia na hata maelfu. Kuimarika kwa uanguaji, kupungua kwa vifo vya vifaranga na mifumo bora kukabidhi vifaranga kwa wanaonufaika, kunasaidia kukuza jamii kimaendeleo.
Baadhi ya vikundi vinatengeneza vifaa vya kuangulia vifaranga na kufuga na kulima vyanzo mbadala vya protini, ikiwemo nzi aina ya Black Soldier Fly (BSF) na mmea wa majini wa Azolla, kupunguza gharama za chakula cha kuku.
Bw Marchisio alisema kilimo cha mabustani ya nyumbani, uvunaji maji ya mvua na upandaji miti, pia vinasaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Biashara za kuku zinazoendeshwa na vijana zinashirikisha uhifadhi wa mazingira kupitia mipango kama vile “Trees for Chicks”.
Ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa malisho
Ufugaji wa nyuki unaongeza mapato ya vikundi vilivyonufaika na mradi huo, kupitia uwekezaji katika mizinga, vifaa vya kurina asali na mashine za kuchakata bidhaa hiyo.
“Uwekezaji katika shughuli tofauti kama vile ufugaji wa nyuki, kuku na samaki huongeza vyanzo vya mapato na kupunguza utegemeaji wa shughuli moja ya kilimo,” ripoti ya mradi huo inaeleza.

Vikundi hugawana mapato au kuyawekeza tena katika biashara zao. Baadhi, pia, vimeanzisha vitalu vya miche ya miti na kupanua shughuli za ufugaji wa samaki na kuku. Hali kadhalika, wanahimizwa kutumia vyanzo mbadala vya nishati, ikiwemo nishati ya jua, sola, ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuhifadhi mazingira. Katika ufugaji wa wanyama wadogo, wafugaji wanaanzisha miradi ya mifugo walioboreshwa, wakiwemo kondoo aina ya Dorper.
Wanawake na vikundi vilvyochanganyika vya wakulima na wafugaji vinatumia mafunzo ya afya ya mifugo, lishe na masoko kuimarisha biashara zao. Isitoshe, vinatumia mfumo wa Gender Action Learning System (GALS) kuhimiza ushirikiano katika familia na kuhakikisha manufaa ya shughuli za kilimo yanagawanywa kwa haki na usawa.
Uzalishaji wa malisho ya mifugo pia unaimarika, huku maghala ya kisasa ya nyasi yakisaidia kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuhakikisha malisho yanapatikana wakati wa kiangazi.
Ripoti ya mradi huo inaeleza kuwa kikundi kimoja kiliandikisha idadi kubwa ya mavuno kuwahi kushuhudiwa, kikizalisha maelfu ya marobota (bales) ya nyasi, pamoja na kiasi kikubwa cha mbegu bora. Mafanikio hayo yamebuni ajira na kuweka msingi faafu wa uwekezaji katika uboreshaji wa mifugo na kuongeza thamani ya bidhaa.
Vijana, pia, wanajihusisha zaidi na ufugaji wa kibiashara, huku vikundi vikikodisha au kununua ardhi, kuongeza kiwango cha mifugo na kuweka malengo ya kufuga mifugo yenye nasaba bora.
Mafunzo kuhusu usimamizi wa biashara, uwekaji rekodi na masoko, yanawasaidia kusimamia shughuli zao kitaalamu. Kupitia uhamasishaji, mashamba ya mafunzo (demonstration farms) na kubadilishana maarifa, Kenya Livestock Commercialization Project inalenga kugeuza ufugaji kutoka shughuli ya kujikimu pekee kuwa biashara zinazozalisha mapato ya kutegemewa, kubuni ajira na kusambaza bidhaa sokoni.