Dimba

Junior Starlets kuoiga kambi Uhispania kujiandaa kwa Kombe la Dunia

Na TOTO AREGE October 2nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Timu ya taifa ya soka ya mabinti wasiozidi miaka 17, Junior Starlets, ilitarajiwa kuondoka nchini Ijumaa kuelekea Uhispania kwa kambi ya maandalizi ya Kombe la Dunia litakalofanyika Morocco kuanzia Oktoba 17 hadi Novemba 7.

Kenya itashiriki kwa mara ya pili mashindano hayo baada ya kuandikisha historia 2024 kwa kuwa timu ya kwanza ya soka nchini kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

Kocha Mildred Cheche alisema kambi ya Uhispania itakuwa muhimu kwa kikosi chake kabla ya kuanza kwa mashindano hayo yatakayoshirikisha mataifa 24.

“Tutacheza mechi kadhaa za kirafiki nchini Uhispania, zikiwemo dhidi ya Australia na klabu za Real Betis na Cadiz. Tunatumai maandalizi haya yatatusaidia,” alisema Cheche wakati wa mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Annex, Nairobi jana.

Kenya imepangwa Kundi E pamoja na China, Marekani na Samoa. Starlets itaanza kampeni yake dhidi ya China Oktoba 19, kabla ya kukabiliana na Marekani Oktoba 22 na kumalizia mechi za makundi dhidi ya Samoa Oktoba 25.

Mechi zote zitachezwa katika Akademia ya Soka ya Mohammed VI, katika mji wa Salé, Morocco.

Cheche alisema uzoefu waliopata wachezaji wake katika fainali za 2024 nchini Jamhuri ya Dominican utawasaidia kukabiliana na wapinzani wao.

“Safari hii tunajua cha kutarajia. Tumechambua wapinzani wetu na tunawaandaa wachezaji kufanya maamuzi bora uwanjani,” alisema.

Starlets ilifuzu kwa mashindano hayo baada ya kuicharaza Namibia kwa jumla ya mabao 7-1, kuiondoa Uganda kwa kanuni ya mabao ya ugenini baada ya sare ya 1-1, kisha kuilaza Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 5-1.

Mshambuliaji Mwanakombo Bakari anatarajiwa kujiunga na kikosi hicho Morocco Oktoba 15 baada ya kupata ufadhili wa masomo katika Spire Academy, Marekani.

Hata hivyo, beki Faith Boke bado anauguza jeraha, huku Cheche akitumai atakuwa fiti kabla ya mashindano kuanza.

Nahodha Berveline Awuor alisema Starlets inalenga kuvuka hatua ya makundi baada ya kushinda mechi moja katika fainali za 2024.

“Safari hii tunataka kushinda mechi nyingi zaidi na kufika mbali,” alisema Awuor.

Kenya ni miongoni mwa mataifa matano ya Afrika yatakayoshiriki, pamoja na Morocco, Ghana, Zambia na Nigeria.