Ripoti yaonya kuhusu hatari ya vipodozi kwa macho
FASHONI
BIDHAA za urembo zinazotumika kila siku na waraibu wa vipodozi, mapambo na mitindo ya urembo ni kiini cha maelfu wanaoishia hospitalini kwa majeraha anuai, utafiti mpya unaonya.
Urembo sasa huenda ukakugharimu uwezo wako wa kuona, wataalam wanatahadharisha wakisisitiza haja ya kuwa makini unapotumia bidhaa mbalimbali za kuboresha mwonekano wako.
Maelfu ya watu hufika hospitalini kila mwaka wakiwa na majeraha ya macho yanayotokana na matumizi ya vifaa vya urembo na vipodozi, kulingana na ripoti mpya.
Ripoti iliwasilishwa katika kongamano la kila mwaka la American Academy of Ophthalmology (AAO).
Ilitaja vifaa hivi kujumuisha vipodozi vya macho, mapambo ya kutia nakshi kucha, bidhaa za nywele, gundi ya kope, spray ya uso na vifaa vinavyotumia moto kupamba nywele.
Vipodozi huenda vikaonekana kuwa na tishio ndogo kwa sababu ni vifaa vinavyotumika nyumbani kila siku.
Hata hivyo, “vinapotagusana na macho, hasa bidhaa zinazosheheni kemikali au vifaa vyenye moto wa kiwango cha juu, vinaweza kusababisha jeraha kubwa,” wanaonya wataalam.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Missouri, Kansa City walichanganua data kutoka kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Kuangazia Majeraha kwenye udadisi uliofanyika kati ya 2005 na 2024.
Walibaini kuwa watu wasiopungua 42,500 waliishia vitengo vya dharura katika hospitalini wakiugua majeraha ya macho yaliyotokana na vipodozi na vifaa vya kujitunza nafsi.
Wanawake na wasichana walijumuisha waathiriwa wanne kwa kila watano (asilimia 82) ya majeraha haya, kulingana na ripoti.
Ingawa umri wa jumla kwa wagonjwa ulikuwa miaka 24, watoto wenye umri wa miaka minne na kwenda chini waliathirika vilevile wakijumuisha karibu robo ya visa vya majeraha kutokana na vipodozi, walisema watafiti.
Mtindo wa majeraha ulitofautiana kutegemea umri wa mgonjwa. Kuchomeka na kemikali kulijumuisha asilimia 46 ya majeraha kwa macho ya wagonjwa wachanga wenye umri chini ya miaka 18, ikilinganishwa na chini ya asilimia moja ya watu wazima, utafiti ulionyesha.
Miongoni mwa majeraha yote ya kuchomeka na kemikali yaliyotibuiwa, asilimia 83 ilihusishwa na mtoto kushika kifaa cha kujipodoa.
Vipodozi hivi vilijumuisha bidhaa za kutunza ngozi na manukato (asilimia 40), bidhaa za kutia nakshi kucha (asilimia 22) spray na shampoo (asilimia 22).
Miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka minne na kwenda chini, asilimia 70 walijeruhiwa walipokuwa wakitumia vifaa au bidhaa za vipodozi wakiwa pekee yao bila uangalizi.
Watu wazima, kwa upande mwingine, aghalabu walipata majeraha ya kukatwa, vidonda au kukwaruzwa kwenye macho yao.
Majeraha kwa watu wazima yalijumuisha majeraha ya macho (asilimia 56) na majeraha ya kuchomeka macho (asilimia 22), kulingana na ripoti hiyo.
Wataalam wanasisitiza umuhimu wa kumakinika kuhusu uhifadhi wa vipodozi na vifaa vya kujitunza binafsi ili kuhakikisha havifikiwi na watoto.
“Kwa watoto, inamaanisha kusisitiza uhifadhi kwa njia salama na kuzuia kufikia bidhaa za urembo bila uangalizi hasa bidhaa majimaji na spray,” walisema wataalam.
Vijana chipukizi na watu wazima wanashauriwa kuzingatia mbinu salama za kutumia na mapambo ya moto ili kupunguza tishio la majeraha.