Saudi Arabia yapiga marufuku safari za Wakenya kutokana na Ebola
Saudi Arabia imepiga marufuku raia wake kusafiri Kenya na kusitisha utoaji wa visa kwa wasafiri kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufuatia kuthibitishwa kwa ugonjwa wa Ebola, hatua inayoongeza wasiwasi kuhusu athari za kimataifa za ugonjwa huo.
Hatua hiyo iliyotangazwa Ijumaa, Oktoba 30, inajumuisha pia kuwazuia wasafiri waliotembelea Kenya katika siku 21 zilizotangulia kuingia katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Saudi Arabia imejiunga na El Salvador ambayo tayari imezuia wasafiri kutoka Kenya na mataifa mengine saba ya Afrika.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), marufuku hiyo inalenga kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo katika taifa hilo.
Mamlaka ya afya ya Saudi Arabia, Weqaya, imesema hali ya afya nchini humo ni shwari na inaendelea kufuatiliwa.
Hatua hizo zimeibua hofu kuhusu athari zinazoweza kukumba Kenya katika sekta za utalii, biashara na usafiri wa kimataifa.
El Salvador ilitangaza kuwa wasafiri waliotoka au kupitia Kenya, Angola, Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Uganda hawataruhusiwa kuingia nchini humo.
Mwanahabari wa CNN Larry Madowo hivi majuzi alifichua kuwa ombi lake la kupata kibali maalumu cha kuingia El Salvador lilikataliwa kutokana na maagizo hayo.
Nchi nyingine zimechagua kuimarisha ukaguzi wa afya badala ya kupiga marufuku wasafiri. Korea Kusini iliiongeza Kenya katika orodha ya mataifa ambayo wasafiri wake wanahitaji kufanyiwa uchunguzi mkali wa afya kuanzia Oktoba 20.
Wasafiri kutoka Kenya wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu hali yao ya afya na wanaweza kufuatiliwa kwa siku 21, ambazo ni kipindi cha kupevuka kwa virusi vya Ebola.
Amerika pia iliwaonya raia wake kufikiria upya mipango ya kusafiri Kenya, huku ikiimarisha ukaguzi wa wasafiri kutoka eneo hili.
Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya dhidi ya mataifa kufunga mipaka au kuzuia biashara kutokana na mlipuko huo.
Katika taarifa ya Oktoba 23, WHO ilisema inapendekeza mataifa kuimarisha ushirikiano, ufuatiliaji wa afya, upimaji na kuwafuatilia watu waliokutana na wagonjwa badala ya kuweka vizuizi vya safari.
Kenya ilirekodi kisa chake cha kwanza cha Ebola aina ya Bundibugyo baada ya mwanaume aliyekuwa amesafiri kutoka DRC kupitia Uganda kufariki Oktoba 5.
Kufikia Oktoba 30, visa tisa vilikuwa vimethibitishwa na watu wawili kufariki. Wagonjwa wengine walikuwa jamaa wa mwathiriwa wa kwanza na wahudumu wa afya waliomhudumia.
Katibu katika Idara ya Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema Kenya ilikuwa imepita siku 10 bila kuripoti maambukizi mapya.
Alisema serikali ilikuwa imeimarisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo kwa kushirikiana na serikali za kaunti na washirika wa maendeleo.
Wizara ya Afya pia ilisema watu waliokuwa wamekutana na wagonjwa na kukamilisha siku 21 za ufuatiliaji bila kuonyesha dalili waliachiliwa hatua kwa hatua. Wengine wanatarajiwa kukamilisha ufuatiliaji kufikia Novemba 11.
Ebola ni ugonjwa hatari unaosambazwa kwa kugusana moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa.
Dalili zake ni pamoja na homa, kutapika na kuharisha, huku wagonjwa mahututi wakikumbwa na kutokwa damu ndani au nje ya mwili.