Kalonzo asihi viongozi wa Ukambani walinde ngome yake
KIONGOZI wa chama cha Wiper Patriotic Front (WPF), Kalonzo Musyoka, amewataka washirika wake wa kisiasa kuungana na kulinda ngome yake ya Ukambani dhidi ya juhudi za Rais William Ruto kuongeza ushawishi wake katika eneo hilo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Bw Musyoka, ambaye anapigania tiketi ya urais ya upinzani, amewashutumu viongozi wake kwa kushindwa kukabiliana na washirika wa Rais Ruto wanaofanya kampeni katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni.
Akizungumza Jumamosi katika hafla ya ufunguzi wa makazi ya Seneta wa Machakos Agnes Kavindu katika eneo la Mua Hills, Bw Musyoka alisema washirika wake wanapaswa kufanya kazi pamoja badala ya kila mmoja kujipigia debe kivyake.
Alitaja kundi la watu watano wanaoendesha kampeni pamoja katika eneo la Machakos, likiongozwa na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, na kuwataka viongozi wake kuiga mtindo huo.
“Badala ya kuwakabili ilhali wananchi wako nyuma yako, kila mtu anafanya kampeni kivyake. Amkeni na mshirikiane ili mniruhusu kuendeleza kampeni katika maeneo mengine ya nchi,” akasema Bw Musyoka.
Alisema kutohudhuria kwa wingi kwa washirika wake katika uzinduzi wa sekretarieti ya vuguvugu la Linda Mwananchi jijini Nairobi kumeathiri juhudi zake za kuonyesha kuwa upinzani umeungana kumuunga mkono.
Mzozo huo unajiri wakati ambapo Bw Musyoka anakabiliwa na ushindani wa ndani ya Wiper. Machakos, kwa mfano, imekuwa na migawanyiko kati ya Bi Kavindu na Gavana Wavinya Ndeti.
Hali imechangiwa na kuingia kwa afisa mkuu wa zamani wa afya wa kaunti hiyo Daniel Yumbya, wakili Musyoka Kala na afisa wa ardhi Nathaniel Nganga katika kinyang’anyiro cha tiketi ya Wiper ya useneta. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua katika kinyang’anyiro hicho pia kumeongeza ushindani.
Mbunge wa Kilome, Thaddeus Nzambia, alisema Machakos imeathiriwa zaidi na juhudi za Rais Ruto kujenga ushawishi Ukambani. Alisema kati ya wabunge wanane wa kaunti hiyo, watano wanaunga mkono Rais, huku wawili pekee wakimuunga mkono Bw Musyoka.
Mbunge wa Mavoko Patrick Makau amejitenga na Bw Musyoka na kujiunga na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Bw Nzambia alitaja Makueni pekee kama eneo ambalo viongozi wake bado wako na Bw Musyoka, Kulingana naye, ni mbunge mmoja pekee anayeunga mkono Rais Ruto.
Bw Musyoka pia anakabiliwa na ushindani wa tiketi za Wiper katika Kitui, ambako Seneta Enoch Wambua, Mwakilishi wa Wanawake Irene Kasalu na Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu wanawania tiketi ya chama kuwania ugavana. Kuingia kwa aliyekuwa Gavana Charity Ngilu kumeongeza ushindani zaidi japo hatarajii kutumia Wiper.
Bw Musyoka amekuwa akiahidi kuwa uteuzi wa Wiper utakuwa huru na wa haki, huku akiwataka washirika wake kutatua tofauti zao na kuimarisha chama.