HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Majonzi walimu kufa wakielekea harusini

Na TITUS OMINDE November 2nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SAFARI ya walimu kutoka Kaunti ndogo ya Matete, Kaunti ya Kakamega, kuenda kusherehekea harusi ya mtoto wa mwenzao iligeuka msiba baada ya watu sita kufariki katika ajali ya barabarani.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa manane wikendi karibu na Burnt Forest, kwenye barabara kuu ya Eldoret-Nakuru.

Miongoni mwa waliofariki ni Janet Andabwa, kaimu mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Chavere, ambaye kifo chake kimeiacha familia yake katika majonzi tele.

Mumewe, Geoffrey Besele, ambaye pia ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Tande, alisema mkewe aliondoka nyumbani akiwa na furaha baada ya kukamilisha kusimamia na kutathmini mitihani ya KJSEA.

Alisema Bi Andabwa aliagana naye na kuanza safari yake kuelekea Nairobi mnamo saa mbili usiku, baada ya kuchukuliwa na walimu wenzake katika kituo cha kibiashara cha Kaburengu.

Hata hivyo, furaha hiyo ilikatizwa alfajiri baada ya kupokea simu iliyomfahamisha kuhusu ajali hiyo.

“Nilipokea simu ya kuhuzunisha saa kumi alfajiri kwamba alikuwa amepata ajali huko Burnt Forest,” akasema Bw Besele huku akishindwa kuzuia machozi katika Kituo cha Polisi cha Tarakwa, ambako mabaki ya magari yaliyohusika kwenye ajali yalikuwa yamepelekwa.

Mbali na Bi Andabwa, waliofariki ni mwalimu mwengine kutoka Shule ya St Mikasa Girls, mwalimu wa Chavere, binti wa mwalimu mmoja wa eneo hilo na mfanyabiashara maarufu katika soko la Matete.

Walimu na familia zao wameathirika pakubwa kutokana na mkasa huo.

Watu wengine watano waliojeruhiwa wanaendelea kupokea matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH), Eldoret.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Wilberforce Sichirani, alisema ajali hiyo ilihusisha lori kubwa lililokuwa likisafirisha saruji na kokoto kuelekea Eldoret.

Alisema lori hilo liligongana na gari la abiria la North Rift Shuttle kabla ya kugonga magari mengine matatu.

Abiria waliokuwa ndani ya gari aina ya Probox na gari jingine la uchukuzi wa umma pia waliathirika katika ajali hiyo.

Mkasa huo umeibua tena wasiwasi kuhusu usalama katika barabara kuu ya Eldoret-Nakuru, miezi michache tu baada ya ajali nyingine katika eneo hatari la Mlima Punda kuua watu saba, wakiwemo wanafunzi wawili waliokuwa wakisafiri kuelekea nyumbani kwa likizo.

Mkazi wa Koriomat, Ben Lelei, alisema eneo hilo limekuwa hatari kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva wa malori yanayosafirisha mizigo.

Alilalamikia pia watu waliotumia vurugu zilizotokana na ajali hiyo kuwaibia abiria badala ya kuwasaidia manusura.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba huku baadhi yetu tukijitahidi kuwaokoa manusura, wengine walikuwa wakiiba mali za abiria waliofariki na walionurika,” akasema.