Usalama wakazwa KCSE ikianza rasmi
MTIHANI wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka huu wa 2026 ulianza rasmi jana kote nchini huku maelfu ya watahiniwa wakianza kufanya mitihani yao katika mazingira ya ulinzi mkali na onyo kali dhidi ya udanganyifu.
Mwaka huu, watahiniwa, wasimamizi na maafisa wengine wamepigwa marufuku kuingia katika vyumba vya mitihani wakiwa wamevaa saa za mikononi, zikiwemo saa za kawaida na za kisasa.
Watahiniwa wanatarajiwa kutumia saa za ukutani zilizowekwa katika vyumba vya mitihani.
Katika Moyale, Marsabit, watahiniwa 220 kutoka shule mbili za mpakani walihamishwa hadi shule nyingine baada ya risasi zilizopotea kutoka mapigano upande wa Ethiopia kulenga shule zao.
Watahiniwa wa shule za mseto za Sessi na St Mary walihamishiwa shule za msingi zilizo salama zaidi. Jumla ya watahiniwa 1,443 wanafanya mitihani katika vituo 12 vya eneo hilo huku wanajeshi KDF na maafisa wa usalama wa mipaka wakiongeza doria.
Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC), Prof Julius Nyabundi, alisema kufikia Jumatatu asubuhi hakukuwa na taarifa za udanganyifu. Alisema huu ni mtihani wa pili kutoka mwisho kusimamiwa na KNEC kabla ya mabadiliko ya mfumo wa mtaala.
Uasin Gishu, watahiniwa 22,593 walianza mtihani katika vituo 246. Maafisa walipiga marufuku saa za mikononi, mavazi yasiyo sare za shule na watu wasioidhinishwa kuingia vyumba vya mitihani.
Turkana, zaidi ya watahiniwa 7,000 katika vituo 68 walianza mitihani huku wakuu wa shule wakiomba ulinzi zaidi katika maeneo yanayokumbwa na ujangili. Serikali kuu na ile ya kaunti pia inafuatilia uwezekano wa mafuriko kuathiri usafirishaji wa karatasi za mitihani.
Baringo ilisajili watahiniwa 16,549 katika vituo zaidi ya 196, huku Trans Nzoia ikiwa na 28,353 katika vituo 253. Maafisa walisema zoezi lilianza bila matatizo makubwa.
Nyeri, watahiniwa wanne wanafanyia mitihani hospitalini kutokana na matatizo ya kiafya. Bomet pia ina watahiniwa watatu hospitalini, wakiwemo wawili wenye ujauzito.
Murang’a iliwasajili watahiniwa 32,487, lakini kukazuka wasiwasi kuhusu karibu wanafunzi 600 waliodaiwa kuacha shule tangu walipojiunga na Kidato cha Kwanza. Baadhi ya watahiniwa pia walilalamikia kupewa chakula kidogo kutokana na kuchelewa kwa fedha za serikali.
Kisumu ilisajili watahiniwa 25,849 katika shule 246, huku Kisii ikiimarisha usalama katika vituo vyake 45.
Katika eneo la Pwani, watahiniwa 63,415 walianza mitihani. Kilifi ilikuwa na 25,617, Mombasa 12,187, Kwale 12,171, Taita Taveta 7,994, Tana River 3,082 na Lamu 2,364.
Huko Lamu, mitihani ilianza kwa utulivu hata katika maeneo yenye changamoto za kiusalama ya Msiti wa Boni na Kiunga, mpakani mwa Kenya na Somalia.
Kwa ujumla, maafisa wa elimu na usalama walisema maandalizi yalikuwa yamekamilika, huku wakiahidi kuhakikisha mitihani inaendeshwa kwa usalama na bila udanganyifu.