HabariHabari za Kitaifa

Wanawake Kenya sasa wanataka watoto wawili -utafiti

Na Angela Oketch November 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

IDADI ya watoto ambao mwanamke huzaa nchini Kenya inatofautiana pakubwa kulingana na anapoishi, kiwango chake cha elimu na hali yake ya kiuchumi, huku wanawake wengi wakisema wangependa kupata watoto wawili pekee.

Ripoti mpya ya Utafiti wa Afya  kuhusu Idadi ya Watu Kenya (KDHS) ya mwaka 2025–2026 inaonyesha kuwa mwanamke wa kaunti ya Embu huzaa wastani wa watoto 2.2 katika maisha yake, ikilinganishwa na watoto 6.8 kwa mwanamke wa Mandera.

Tofauti hiyo inaonyesha pengo kubwa la uzazi nchini, licha ya Kenya kupiga hatua katika kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na kila mwanamke.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha uzazi nchini kimeshuka hadi watoto 3.1 kwa kila mwanamke, kutoka 3.4 mwaka 2022 na 6.7 mwaka 1988–89.

Hata hivyo, idadi ya watoto imeanza kupungua, huku matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi na mahitaji ambayo hayajatimizwa yakiongezeka.

Wanawake wengi walisema wangependa kupata watoto wawili, lakini wastani wa kitaifa bado ni 3.1.

Hali ni tofauti katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya, ambako wanawake wanapata watoto wengi zaidi na matumizi ya njia za kisasa za kisasa za kupanga uzazi ni madogo mno.

Mandera inaongoza kwa kiwango cha juu kwa watoto 6.8 kwa kila mwanamke, ikifuatiwa na Wajir (5.8), Tana River (5.7), Turkana (5.6), Garissa (5.3), West Pokot (5.1) na Samburu (5.0).

Kwa upande mwingine, Embu ina kiwango cha chini zaidi cha watoto 2.2, ikifuatiwa na Kiambu na Mombasa zenye 2.3 kila moja. Kericho na Nairobi zina kiwango cha 2.6.

Elimu pia inaonekana kuwa na mchango mkubwa katika idadi ya watoto ambao mwanamke huzaa.

Wanawake ambao hawajasoma wanapata wastani wa watoto 5.4, ikilinganishwa na 3.6 kwa walio na elimu ya msingi, 3.0 kwa wenye elimu ya sekondari na 2.7 kwa walioendelea na masomo baada ya sekondari.

Hali hiyo pia inajitokeza katika hali ya kiuchumi. Wanawake kutoka familia maskini zaidi wana wastani wa watoto 4.5, huku wale kutoka familia tajiri zaidi wakiwa na 2.3.

Ripoti inaonyesha pia kuwa wanawake wameanza kupata watoto wakiwa na umri mkubwa zaidi. Hapo awali, wanawake wengi walikuwa wakijifungua zaidi wakiwa na umri wa miaka 20 hadi 24, lakini sasa kundi linaloongoza ni la miaka 25 hadi 29.

Vilevile, mimba miongoni mwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 zimepungua. Asilimia ya wasichana katika kundi hilo ambao wamewahi kupata mimba imeshuka kutoka 14.8 mwaka 2022 hadi 11.9 sasa.

Serikali inalenga kuongeza matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi hadi asilimia 64 ifikapo 2030 na kupunguza mahitaji ambayo hayajatimizwa hadi asilimia 10.

Mandera ina kiwango cha chini zaidi cha matumizi, chini ya asilimia moja, huku Wajir ikiwa na asilimia moja na Garissa asilimia tano.

Katika kaunti za Nyamira, Nandi na Bomet, wanawake wanapata watoto 1.1 zaidi ya idadi wanayotamani. Hali hiyo inaonyesha kuwa kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa kutahitaji kuboresha upatikanaji wa huduma za kupanga uzazi na elimu kuhusu afya ya uzazi.