Visa vya wahalifu kushambulia polisi, wanajeshi zazua hofu
MATUKIO mawili tofauti ya mapigano kati ya maafisa wa usalama na washukiwa wa uhalifu yamezua wasiwasi kuhusu usalama wa polisi na wanajeshi, huku bunduki zikiendelea kuibwa na magenge ya wahalifu.
Katika tukio la kwanza, afisa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, baada ya makabiliano yaliyotokea Jumapili, Novemba 1.
Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Kahawa Sukari walikuwa kwenye doria mwendo wa saa saba usiku walipopokea taarifa kutoka kwa mwananchi kuhusu wanaume wawili waliokuwa na silaha na kutishia wakazi wa Covo, karibu na Magunas.
Polisi waliwafuata washukiwa hao na kuwaamuru wasimame, lakini mmoja wao anadaiwa kutoa bastola na kuwafyatulia risasi maafisa hao, waliolazimika kujibu mashambulizi.
“Mshukiwa aliyetoa bunduki alipigwa risasi kifuani na mkono wa kulia. Alikimbizwa katika Hospitali ya Ruiru Level 4 akiwa katika hali mahututi lakini baadaye akafariki akipokea matibabu,” ilisema ripoti hiyo.
Polisi walipata bastola aina ya Jericho iliyokuwa na risasi 12 pamoja na maganda mawili ya risasi zilizokuwa zimefyatuliwa. Pia walipata kitambulisho cha KDF kilichokuwa na jina la marehemu, Munene Antony, 33.
Mshukiwa aliyenusurika anadaiwa kuwaambia wachunguzi kuwa bastola hiyo ilikuwa ya kakake ambaye ni polisi. Uchunguzi unaendelea kubaini umiliki wa silaha hiyo.
Wakati huohuo, maafisa wawili wa polisi kutoka Kituo cha Ruai walijeruhiwa vibaya Jumatatu usiku baada ya kushambuliwa na genge la wanaume waliokuwa wameabiri pikipiki.
Washambuliaji hao waliiba bunduki mbili aina ya AK-47, kila moja ikiwa na risasi 30.
Maafisa hao, Corporal John Maritim na Corporal Felistus Tuitoek, walipata majeraha kichwani na mikononi baada ya kushambuliwa kwa kitu chenye makali.
Walipata matibabu katika Hospitali ya Reale, Utawala, huku polisi wakianzisha msako wa kuwakamata washukiwa na kurejesha silaha hizo.
Tukio hilo linaongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa bunduki hizo kutumiwa katika uhalifu mwingine au mashambulizi dhidi ya raia na maafisa wa usalama.
Mnamo Oktoba 26, genge lilishambulia maafisa waliokuwa wakilinda kituo cha ukusanyaji ushuru Kaunti ya Mombasa, Likoni, na kumuua afisa mmoja wa kaunti huku wengine watatu wakijeruhiwa.
Washambuliaji waliiba bunduki ya AK-47 kutoka kwa afisa wa utawala, ambayo baadaye ilitumika kumpiga risasi afisa huyo wa kaunti.
Mnamo Machi, genge jingine lilishambulia polisi aliyekuwa akilinda eneo la viwanda la Bonje, Jomvu, na kumuibia bunduki ya AK-47 pamoja na simu.
Matukio hayo yanajiri huku kukiwa na ripoti za mivutano kati ya polisi na wanajeshi. mnamo Septemba, maafisa hao walikabiliana katika kizuizi cha barabarani karibu na Chuo Kikuu cha Turkana, Lodwar, na baadaye katika Kituo cha Polisi cha Lodwar.
Tukio jingine la mzozo kati ya polisi na wanajeshi liliripotiwa katika kivuko cha feri cha Likoni, Mombasa, mwezi huohuo.
Matukio haya yanaibua maswali kuhusu ushirikiano kati ya idara za usalama, nidhamu kazini na silaha za serikali kuangukia mikononi mwa wahalifu.