HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Viongozi wa Wiper watishia kujitenga na upinzani kuhusu tiketi ya urais

Na KEVIN MUTAI November 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa chama cha Wiper katika eneo la Pwani wametishia kujiondoa katika muungano wa upinzani na kumuunga mkono kiongozi wao Kalonzo Musyoka kuwania urais kivyake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 iwapo hatapewa tiketi ya pamoja ya urais.

Viongozi hao wa mashinani wamesisitiza kuwa wakati umefika kwa Bw Musyoka kupewa nafasi ya kuwania urais badala ya kuendelea kuunga mkono wagombeaji wengine au kukubali kuwa mgombea mwenza.

Pia walipuuza madai kwamba aliyekuwa makamu wa rais anaweza kushirikiana kisiasa na Rais William Ruto katika uchaguzi ujao, wakisema wawili hao hawana uwezekano wa kuunda muungano.

Mwanachama wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Wiper, Omar Twaha, alidai kuwa Kalonzo amekuwa akidhulumiwa ndani ya upinzani licha ya mchango wake katika juhudi za kuunganisha viongozi wanaopinga utawala wa Rais Ruto.

Hata hivyo, Bw Twaha alisema chama hicho hakina nia ya kuvunja muungano wa upinzani, bali kinataka viongozi waheshimiane na kumpa kila mmoja nafasi sawa katika mazungumzo kuhusu mgombeaji wa urais.

“Iwapo tutamsimamisha Kalonzo kama chama, tutavunja upinzani, na hilo si lengo letu. Lengo letu ni moja, kumuondoa Rais William Ruto mamlakani. Kwa hivyo, ni lazima tuheshimiane,” alisema.

Mwenyekiti wa Wiper Pwani, John Chamia, alipuuza madai kwamba Kalonzo anaweza kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto, akisisitiza kuwa wawili hao hawawezi kushirikiana kisiasa.

“Anayesema Kalonzo atakuwa naibu wa Ruto anaota. Hatuwezi hata kufanya mazungumzo naye kwa sababu Ruto na Kalonzo hawawezi kuwa pamoja,” alisema Bw Chamia.

Viongozi hao walisema iwapo Kalonzo atapuuzwa katika mchakato wa kumchagua mgombeaji wa urais wa upinzani, watamlazimisha kuwania kiti hicho nje ya muungano.

Walisema Kalonzo alikuwa akimuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika chaguzi zilizopita na sasa ni wakati wa viongozi wengine wa upinzani kulipa fadhila hiyo.

“Kalonzo hakuzaliwa kuwa mgombea mwenza katika kila uchaguzi. Alimuunga mkono Raila Odinga na sasa ni wakati wa wao kumuunga mkono. Tunamwambia Kalonzo kwamba hatutaki kusikia akiunga mkono mtu mwingine. Tunataka kumuona kwenye karatasi ya kura,” alisema mmoja wa viongozi hao.

Msimamo huo unajiri huku kukiwa na ushindani mkali ndani ya upinzani kuhusu nani atabeba bendera ya urais katika uchaguzi wa 2027.

Miongoni mwa wanaotajwa ni Kalonzo, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, ambaye pia anaongoza chama cha Jubilee.

Naibu kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Cleophas Malala, amekuwa akimhimiza Kalonzo kuachana na azma yake ya urais na kumuunga mkono Sifuna.

Bw Malala anasema Sifuna, mwenye umri wa miaka 45, anawakilisha kizazi kipya cha uongozi na anafaa kupewa nafasi ya kuongoza nchi, huku mwanasiasa mkongwe akichaguliwa kuwa mgombea mwenza.

“Ninataka Kalonzo kuiga mfumo wa Obama na Biden. Tumuunge mkono Sifuna, mwenye umri wa miaka 45, kuwa mgombeaji wa urais wa upinzani, kisha tutafute mwanasiasa mkongwe awe mgombea mwenza wake,” alisema.

Hata hivyo, viongozi wa Wiper Pwani walisema Kalonzo ana uzoefu wa kutosha kuongoza nchi na hawatakubali azma yake ya urais kupuuzwa kwa kisingizio cha kudumisha umoja.

Pia walidai kuwa baadhi ya watu wanaohusishwa na serikali wanatumia tofauti ndani ya upinzani kujaribu kuudhoofisha kabla ya uchaguzi wa 2027.

Walisema umoja wa upinzani ni muhimu, lakini haupaswi kujengwa kwa kumdharau au kumtenga kiongozi yeyote anayetamani kuwania urais.