Siasa

Wandani wa Sifuna wajipata kwenye mng’ang’anio wa tiketi Bungoma

Na CECIL ODONGO November 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anakabiliwa na kibarua Kaunti ya Bungoma, ambako washirika wake watatu wanang’ang’ania tiketi ya chama cha Linda Mwananchi kuwania ugavana katika uchaguzi wa 2027.

Bw Sifuna ametangaza nia ya kuwania urais 2027 kupitia chama hicho.

Washirika wake Gavana wa zamani Wycliffe Wangamati, Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi na mfanyabiashara Zacharia Barasa nao wanataka ugavana.

Hali ni tofauti na kaunti jirani ya Trans Nzoia, ambako Gavana George Natembeya anaonekana kuwa mgombea mkuu wa Linda Mwananchi.

Bw Wangamati alihudumu kama gavana kati ya 2017 na 2022, kabla ya kushindwa na gavana wa sasa Ken Lusaka.

Bw Wangamati aliunga mkono Azimio, huku Lusaka akiwa katika kambi ya Rais William Ruto.

Bw Wangamati anaamini atapata tiketi ya Linda Mwananchi na kwamba yupo tayari kushiriki mchujo dhidi ya wapinzani wake.

“Nimekuwa nikifanya kampeni na nilichokiona ni kwamba wakazi wa Bungoma wanataka nirudi kuwa gavana kwa sababu ya kazi niliyofanya. Niko tayari kwa mchujo wa Linda Mwananchi,” akasema.

“Gavana ajaye wa Bungoma atatoka Linda Mwananchi. Rekodi yangu ya maendeleo iliweka kiwango cha juu na nataka kurejea nimalize kazi yangu,” akaongeza.

Bw Wangamati alitaja barabara kuu yenye njia mbili Bungoma, Uwanja wa Kanduyi na Hospitali mpya ya kaunti yenye zaidi ya vitanda 300 aliyotekeleza akiwa gavana.

Pia ameahidi kurejesha ufadhili wa masomo kwa zaidi ya wanafunzi 300 aliowasaidia kusoma Amerika.

Bw Sifuna alimkaribisha rasmi Bw Wanyonyi katika chama hicho wakati wa kuwatambulisha viongozi wake jijini Nairobi Ijumaa iliyopita.

Bw Wanyonyi, nduguye Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, anakabiliwa na kibarua cha kujenga upya siasa zake Bungoma baada ya kujikita Nairobi, ambako amekuwa mbunge tangu 2013.

“Bungoma si ufalme wa kuichagua familia ya Wetang’ula kila uchaguzi. Uongozi wao haujasaidia kaunti hii katika maendeleo. Watu hawako tayari kwa uongozi wa familia ya Wetang’ula lakini sisi sasa tumemkubali Sifuna,” akasema.

Bw Wanyonyi alisema aliondoka ODM na kurejea nyumbani kwa wito wa kuhudumia nyumbani.

“Mimi na Sifuna tulikatishwa tamaa ODM, na mliona walivyonitendea Nairobi mnamo 2017. Nilikuwa kipenzi cha wengi na ningekuwa gavana Nairobi, lakini nilikubali kurejea kwenye kiti changu cha ubunge. Sauti ya Mungu imeniambia nirudi nyumbani kuwania Bungoma,” akasema.

“Tunahitaji kuboresha miundombinu katika shule zetu. Nisaidieni kuibadilisha Bungoma, mabadiliko yataonekana katika maisha ya watu wetu,” akasema.

Bw Wanyonyi amekuwa akiwakilisha eneobunge la Westlands tangu 2013, huku siasa zake zikijikita zaidi jijini Nairobi.

Kurejea Bungoma kunamaanisha atahitaji kuwashawishi wapigakura kwamba ana uhusiano na masuala ya kaunti.

Kwa upande wake, Bw Barasa anasema juhudi zake za kutetea mali na maslahi ya umma zinampa msingi wa kuomba uungwaji mkono wa wakazi wengi.

Bw Barasa, mfanyabiashara kutoka Bumula, alieleza kuwa alipigania kurejeshwa kwa ardhi ya uwanja wa ndege kwa umma mahakamani na pia Kiwanda cha sukari cha Nzoia.

“Mimi ni mtu ambaye nimekuwa nikipigania kaunti hii. Nilienda mahakamani na kupigania uwanja wa ndege urejeshwe. Sifuna akipanda ngazi ya uongozi wa kitaifa na mimi kuwa gavana, kaunti hii itaongozwa vyema,” akasema.

Bw Barasa anaamini atapata tiketi ya Linda Mwananchi akisema ameitumikia kaunti kabla ya kuwania wadhifa. Amesema kuwa Mabw Wangamati na Wanyonyi walimpata katika siasa za Bungoma na ana uwezo wa kuwashinda.