Iran wapiga sherehe kumcheka Trump kwa poteza uchaguzi wa nusu muhula
TEHRAN, Iran:
SERIKALI ya Iran imekaribisha kushindwa kwa chama cha Republican cha Rais Donald Trump katika uchaguzi wa katikati ya muhula Amerika, ikisema wapigakura wameonyesha bayana kuwa wanapinga vita vilivyoanzishwa na Washington dhidi ya Tehran.
Democrats walinyakua viti vingi katika Seneti na Bunge la Congress katika uchaguzi wa Jumanne, ushindi ambao umehusishwa na hasira za raia kuhusu gharama ya maisha na uamuzi wa Trump kuanzisha vita vilivyosababisha kupanda kwa bei ya mafuta.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ambaye pia anaongoza mazungumzo ya upatanishi, alisema, kwa kupiga kura namna hiyo, raia wa Amerika wametuma ujumbe wa wazi kuwa hawataki vita hivyo.
“Kwa sababu ya kupanda kwa gharama ya maisha, raia wa Amerika wamesema hawataki vita nasi tunaunga mkono ujumbe huo,” aliandika kwenye mtandao wa X.
Pia alionya Amerika dhidi ya kuishambulia tena Iran na kupuuza maoni ya wananchi wake.
Kiongozi wa Kidini Iran, Mojtaba Khamenei, alisema uhasama wa Amerika dhidi ya nchi yake utaendelea bila kujali chama kitakachokuwa madarakani.
Alionya dhidi ya kuonyesha dalili zozote za kujisalimisha kwa Amerika.
“Amerika inaona mwisho wa utawala wake wa kimataifa kuwa bado uko mbali, lakini sisi tunaona umekaribia,” akasema.
Hata hivyo, maafisa wawili wakuu wa Iran walisema kuwa licha ya kufurahia ushindi wa Democrats, Tehran ina wasiwasi kuwa Trump anaweza kuanzisha mashambulizi mapya ya kijeshi ili kufidia kushindwa kwa chama chake.
Kwa hivyo, Iran bado iko katika hali ya tahadhari ya juu.
Vita vilianza Februari 28 baada ya Amerika na Israel kuishambulia Iran, ambayo ilijibu kwa kushambulia Israel na mataifa ya Ghuba yenye vituo vya kijeshi vya Amerika.
Mapigano hayo yameathiri usafirishaji wa mafuta na gesi duniani, huku shughuli za usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz zikitatizika.
Katika taarifa yake, Khamenei alilaumu sera za Washington kwa kuongeza gharama kwa wananchi wake.