Kinaya cha Gachagua asiyetaka kufundishwa ila naye anafundisha wengine kutafuta kura!
KATIKA siasa, wakati mwingine kinachowachekesha wananchi si wapinzani wa mwanasiasa, bali ni kauli zake mwenyewe.
Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ametupa mfano mzuri wa kinaya hiki.
Akijibu malalamishi ya Justin Muturi na Fred Matiang’i kuhusu tabia yake ya kuwadhalilisha viongozi wengine katika upinzani, Gachagua alisisitiza kwamba hakuna mtu anayepaswa kumfundisha namna ya kutafuta kura.
Kauli hiyo ilionekana kusisitiza uhuru wake wa kisiasa.
Hata hivyo, katika mwelekeo huo huo, aliwakemea wenzake wa upinzani kwa kile alichokitaja kuwa uzembe wa kutafuta kura.
Aliwataka watoke nje, wafanye kazi kwa bidii ya kuzungumza na raia na waache kutarajia kwamba yeye ndiye atakayewaletea kura hadi milangoni mwao.
Hapo ndipo tunapopata kitendawili!
Gachagua hataki kufundishwa namna ya kutafuta kura, lakini yeye hana tatizo la kuwaelekeza wengine namna ya kufanya hivyo.
Je, kanuni ya kutofundishwa inamhusu yeye pekee?
Huenda kinachojitokeza hapa ni zaidi ya tofauti ya mbinu za kisiasa.
Ni swali kuhusu nani anayetaka kuwa na mamlaka ya kuamua namna muungano wa upinzani utakavyosaka kura na nani atakayenufaika zaidi na mpangilio huo.
Wananchi wanapaswa kuwa macho. Wanasiasa wanaweza kutumia lugha ya umoja huku wakifuatilia maslahi yanayotofautiana.
Tusipime viongozi kwa kauli zao tamu pekee, bali pia kwa uthabiti wa misimamo na matendo yao.
Katika siasa, mwalimu anayekataa kufundishwa lakini anataka kufundisha wengine anapaswa kuulizwa: je, anatafuta kura za wote au mamlaka juu ya wote?
- Mwandishi ni msomi na mtafiti wa taaluma za Kiswahili na Mawasiliano