Ichung’wa aibuka na mswada mkali wa kukazia walevi na wauzaji pombe
HUENDA Wakenya wakakosa kununua pombe katika maduka makubwa, mikahawa na maeneo mengine ya umma iwapo Bunge litapitisha mswada mpya unaopendekeza kupandisha umri wa kisheria wa kunywa pombe kutoka miaka 18 hadi 21.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vileo na Udhibiti wa Dawa za Kulevya wa 2026, unaodhaminiwa na Kiongozi wa Wengi, Kimani Ichung’wah, unapendekeza masharti makali kwa watengenezaji, waagizaji na wauzaji wa pombe.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kukabiliana na pombe haramu ambayo imekuwa ikisababisha vifo, upofu na magonjwa ya muda mrefu, huku ikiathiri familia nyingi nchini.
Chini ya kifungu cha 35B, mwenye leseni ya kuuza pombe hataruhusiwa kumruhusu mtu aliye na umri wa chini ya miaka 21 kuingia katika eneo lake, awe peke yake au kuandamana na mtu mzima.
Mswada huo pia unapendekeza maeneo yanayouza pombe yawe umbali wa angalau mita 300 kutoka shule za chekechea, msingi, sekondari na taasisi nyingine za elimu.
Iwapo pendekezo hilo litapitishwa, huenda maelfu ya baa zikafungwa au kulazimika kuhamia maeneo mengine.
Kamati za leseni za pombe za kaunti pia hazitaruhusiwa kutoa vibali vya kuuza pombe katika fukwe za umma, kumbi za sinema, hospitali na vituo vya afya, bustani, viwanja vya michezo, vituo vya mabasi na vituo vya mafuta.
Uuzaji wa pombe pia utapigwa marufuku katika vituo vya reli, bandari na vyombo vya usafiri wa umma kama vile mabasi, treni, ndege, feri na boti.
Maduka makubwa, maduka yanayouza bidhaa zinazohusishwa na watoto, maeneo ya makazi, mikahawa, shule, vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu pia hayatapewa leseni za kuuza pombe.
Aidha, mswada huo unapiga marufuku uuzaji wa pombe kupitia mitandao, huduma za usafirishaji wa vifurushi, kusafirishaji hadi nyumbani au uchuuzi.
Wafanyabiashara ambao tayari wana leseni katika maeneo yaliyopigwa marufuku watapewa muda usiozidi miezi mitatu kuuza bidhaa walizonazo baada ya sheria kuanza kutumika, au hadi leseni zao zitakapoisha, kutegemea ni lipi litakalotangulia.
Mswada huo pia unapendekeza kupiga marufuku maafisa wa serikali za kitaifa na kaunti wanaosimamia sheria hiyo kumiliki au kuendesha biashara ya pombe, moja kwa moja au kupitia watu wengine.
Wamiliki wa majengo hawataruhusiwa kuyapangisha kwa shughuli za kutengeneza, kuhifadhi au kuuza pombe iwapo yako katika maeneo ya makazi au umbali uliopigwa marufuku karibu na shule.
Pia, maeneo yanayouza pombe yatatakiwa kuwa safi na kuwa na vyoo na huduma za usafi za kutosha.
Kamati za leseni zitazingatia idadi ya watu kwa kila kilomita mraba na vibali vilivyotolewa awali ili kuzuia msongamano wa baa katika eneo moja.
Pendekezo la kupandisha umri wa kunywa pombe linajiri wakati takwimu zinaonyesha kuna matumizi makubwa ya vileo miongoni mwa vijana.
Utafiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu, uliotolewa Februari mwaka jana, ulionyesha asilimia 87.3 ya wanafunzi hutumia pombe.
Sigara zilifuata kwa asilimia 64.4 na shisha asilimia 41.2.
Utafiti huo ulihusisha wanafunzi 15,678 kutoka vyuo vikuu vya umma na kibinafsi. Asilimia 66.4 walisema hupata dawa na vileo kupitia marafiki, huku asilimia 59.3 wakitaja vibanda na baa za mitaani kuwa vyanzo vyao.
Takwimu nyingine za Nacada zinaonyesha asilimia 13 ya Wakenya wenye umri wa miaka 15 hadi 65, sawa na takriban watu milioni 4.7, hutumia pombe.
Matumizi ni makubwa zaidi miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 24.
Mswada huo pia unapendekeza kutoza watengenezaji na waagizaji wa pombe ushuru maalumu wa fidia wa Sh2 kwa kila lita inayotengenezwa au kuingizwa nchini.