Utafiti wabaini kaunti ambazo biashara hunawiri kwa urahisi, na hurekodi pato nzuri
WANAOENDESHA biashara katika kaunti za Tana River, Pokot Magharibi, Kajiado na Mandera wana nafasi kubwa ya kupata mapato ya zaidi ya Sh50,000 kwa mwezi kuliko wenzao katika maeneo mengine nchini.
Utafiti mpya wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) unaonyesha kuwa kaunti hizo zinaongoza kwa idadi ya biashara za familia zilizo na mapato yanayozidi kiwango hicho kila mwezi.
Katika utafiti wa Kenya Mini Demographic and Health Survey wa 2025-2026, Tana River inaongoza kwa asilimia 32.3 ya biashara za familia zinazoingiza zaidi ya Sh50,000 kila mwezi.
Hii ina maana kuwa karibu biashara moja kati ya tatu katika kaunti hiyo huingiza kiasi hicho, sawa na angalau Sh600,000 kwa mwaka.
Pokot Magharibi inashika nafasi ya pili kwa asilimia 25.4, ikifuatiwa na Kajiado kwa asilimia 22.3 na Mandera kwa asilimia 20.3.
Hizi ndizo kaunti nne pekee nchini ambako zaidi ya biashara moja kati ya tano zinazoendeshwa na familia huingiza mapato yanayozidi Sh50,000 kwa mwezi.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa biashara za familia katika maeneo hayo zina uwezo mkubwa wa kuzalisha mapato ikilinganishwa na sehemu nyingine za nchi.
KNBS inasema biashara zinazopata wastani wa Sh50,000 au zaidi kwa mwezi zinapatikana katika asilimia 15 ya familia za mijini, ikilinganishwa na asilimia sita ya familia za mashambani.
Utafiti huo ulifanywa kati ya Novemba mwaka jana na Februari 2026, ukihusisha familia 26,380 kote nchini. Ulijikita katika masuala mbalimbali yakiwemo afya, hali ya maisha na shughuli za kiuchumi za familia.
Kaunti nyingine zilizo na biashara nyingi zenye mapato ya zaidi ya Sh50,000 ni Kericho, Nyandarua, Nairobi, Kiambu, Machakos na Marsabit.
Katika Kericho, biashara 13 kati ya 74 zilizoshiriki utafiti zilikuwa zikipata kiasi hicho. Nyandarua ilikuwa na biashara sita kati ya 33, huku Nairobi ikiwa na biashara 226 kati ya 1,338.
Kiambu ilirekodi biashara 58 kati ya 383, Machakos 27 kati ya 179, huku Marsabit ikiwa na asilimia 13.7 ya biashara zilizofanyiwa utafiti.
Licha ya baadhi ya kaunti kuwa na biashara zinazopata mapato makubwa, utafiti unaonyesha kuwa biashara nyingi za familia nchini bado zinapata kiasi kidogo.
KNBS ilisema asilimia 34 ya biashara za familia nchini ziliripoti mapato ya wastani ya Sh5,000 au chini kwa mwezi.
Biashara zilizokuwa zikijizolea kati ya Sh10,000 na Sh19,999 zilichangia asilimia 22, huku zile zilizopata kati ya Sh20,000 na Sh49,999 zikiwa asilimia 21.
Kwale inaongoza kwa kuwa na biashara nyingi zaidi zinazopata chini ya Sh5,000 kwa mwezi, huku asilimia 64.6 ya biashara zilizoshirikishwa katika utafiti katika kaunti hiyo zikiangukia kundi hilo.
Turkana inafuatia kwa asilimia 61.3, Busia ikiwa na asilimia 60.4, Kilifi asilimia 56.2 na Tharaka Nithi asilimia 56.
Kaunti nyingine zenye idadi kubwa ya biashara zinazopata mapato hayo madogo ni Wajir kwa asilimia 54.1, Siaya (53), Bungoma (52.2), Samburu (51.4) na Kakamega (50.2).
Hii ina maana kuwa biashara hizo hupata chini ya Sh170 kwa siku, au chini ya Sh60,000 kwa mwaka.
Utafiti huo pia unaonyesha kuwa familia moja kati ya tano nchini inaendesha biashara, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa lengo la kupata mapato.
Ingawa biashara nyingi za familia ziko maeneo ya mashambani, biashara kubwa kubwa zaidi ziko mijini, ambako robo ya familia zina angalau mwanachama mmoja anayeshughulika na biashara.
Turkana inaongoza kwa asilimia 42.7 ya familia zinazoendesha biashara, ikifuatiwa na Kisumu kwa asilimia 33, Homa Bay (32.1) na Migori (31.8).
KNBS ilibaini pia kuwa uwezekano wa familia kuendesha biashara huongezeka kadiri hali yake ya kiuchumi inavyokuwa bora.
Katika familia zilizo katika kundi la chini zaidi la utajiri, ni asilimia 10 pekee zinazoendesha biashara, ikilinganishwa na asilimia 27 katika kundi la familia tajiri zaidi.
Matokeo haya yanaonyesha tofauti kubwa katika uwezo wa biashara za familia kuzalisha mapato, huku baadhi ya maeneo yakirekodi mafanikio makubwa na mengine yakikabiliwa na mapato duni.