Pambo

Safari ya mapenzi haiishi na ndoa, harusi ni mwanzo tu

Na Benson Matheka November 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Mwanaume anapaswa kuelewa kuwa kumpata mwanamke anayempenda si mwisho wa safari ya mapenzi, bali ni mwanzo wa jukumu la kumtunza, kumheshimu na kuendelea kumthamini.
Kuna mambo mengi kuhusu mwanamke ambayo mwanaume anapaswa kujifunza ili kudumisha uhusiano wenye furaha.
 Kwanza, mwanamke anayempenda mwanaume kwa dhati anaweza kuhisi upweke na huzuni anapokuwa mbali naye. Uwepo wa mpenzi wake humpa faraja na kumfanya ajihisi salama.
Hata hivyo, kupata imani ya mwanamke si jambo la siku moja. Huchukua muda kujenga uaminifu, lakini mwanaume anapovunja imani hiyo kwa uongo, usaliti au tabia zisizofaa, inaweza kuwa vigumu sana kuirejesha.
Wataalamu wa mahusiano wanasema mwanaume anapaswa pia kuelewa kuwa mwanamke ni kama shule ambayo masomo yake hayaishi. Kadiri unavyoishi naye, ndivyo unavyoendelea kugundua mambo mapya kuhusu tabia, hisia, ndoto na matarajio yake.
“Usidhani kuwa cheti cha ndoa ni ruhusa ya kuacha kumtongoza na kumfurahisha. Badala yake, ni kama kibali cha kuendelea kujifunza kuhusu mwenzi wako. Kumwonyesha mapenzi, kumpeleka matembezini, kumsifia na kumjali kunapaswa kuendelea hata baada ya miaka mingi ya ndoa,” asema mtaalamu wa mahusiano Nelly Ikinya.
Anasema mwanamke anaweza kukasirika leo na kufurahi kesho. “Jinsi unavyomchukulia wakati wa hasira inaweza kuamua kama atajihisi kupendwa au kuumizwa zaidi. Epuka matusi, vitisho na maneno ya kumdhalilisha,” aeleza.
Kumbuka kuwa baadhi ya wanawake hukumbuka sana maumivu waliyopitia. Hivyo, kuwa mwangalifu na maneno yako. Unapokosea, omba msamaha badala ya kutafuta sababu za kujitetea.
Pia, usihukumu hisia zake kwa mwonekano wake. Mwanamke anaweza kuonekana mwenye nguvu na furaha mbele ya watu, ilhali moyoni anapitia wakati mgumu. Kuwa rafiki yake wa karibu, msikilize na umpe nafasi ya kueleza yanayomsumbua bila kumkatiza au kumhukumu.
Wanawake wengi pia hupenda kujihisi wa pekee. Mambo madogo kama kumuuliza hali yake, kumshukuru kwa juhudi zake, kumshika mkono au kumwambia anapendeza yanaweza kuleta tofauti kubwa katika uhusiano.
“Usisubiri hadi mwanamke akose nyumbani ndipo utambue umuhimu wake. Uwepo wake unaweza kuwa umefanya maisha yako kuwa rahisi kwa namna ambazo huzitambui. Anapoondoka, ndipo unaweza kugundua mchango wake katika maisha yako,” asema mshauri wa masuala ya ndoa, Jimmy Petu.
Anaongeza kuwa mwanamke anayekupenda anaweza kujitahidi kukufurahisha kwa njia mbalimbali. Hata hivyo, usitumie mapenzi yake kumlazimisha kufanya mambo asiyoyataka. Mapenzi ya kweli yanahitaji hiari, heshima na kuelewana.
Katika masuala ya fedha, asema Petu, mwanaume hapaswi kusubiri mwenzi wake aombe msaada ndipo aone mahitaji yake. Kuwa tayari kumsaidia pale unapoweza, bila kumfanya ajihidi kama ombaomba. Vilevile, msaada wa kifedha haupaswi kutumiwa kama njia ya kumdhibiti.
“Mwanamke anayekupenda na kusimama nawe katika nyakati nzuri na ngumu ni hazina inayopaswa kuthaminiwa. Usimwumize kwa kudhani kuwa atavumilia kila kitu. Upendo unahitaji juhudi za watu wawili,” asema Kinya.