Kenya yaandika historia India Kabaddi
KUFUZU kwa timu zote mbili za wanaume na Wanawake kwa nusu fainali ni hatua kubwa kwa mchezo wa Kabaddi nchini, safari iliyoanza 2014.
Timu hizo zimeweka historia katika michuano ya kwanza ya Jumuiya ya Madola inayoendelea kwenye Uwanja wa Veer Savarkar, Ahmedabad, Gujarat, India.
Timu zote mbili zimefuzu nusu fainali, hatua inayodhihirisha ukuaji wa Kenya Kabaddi kimataifa.
Mashindano hayo yalianza Oktoba 21 na yatakamilika Oktoba 31, 2026, yakileta pamoja mataifa 13 ya Jumuiya ya Madola.
Kikosi cha wanawake kimekuwa moto wa kuotea mbali. Wamemaliza hatua ya makundi bila kupoteza mchezo wowote na kuongoza Kundi B.
Wamewacharaza Bangladesh, Sri Lanka, Uingereza na Scotland. Matokeo yaliyoshangaza zaidi ni kichapo cha 82-6 dhidi ya Uingereza 61-16 dhidi ya Scotland. Pia waliibuka na ushindi finyu wa 23-20 dhidi ya Sri Lanka.
Miongoni mwa nyota waliong’aa ni Lavender Adhiambo aliyetajwa Mshambuliaji Bora (Best Raider), na Faith Cheptoo aliyeibuka Mlinzi Bora (Best Defender) kwenye mechi dhidi ya Scotland.
Chini ya nahodha Mercy Obiero na makamu wake Lizzeanne Owino, wanadada hao sasa wameweka macho kwenye kutwaa kombe.
Wanadada watavaana na Uganda nusu fainali Ieo na mshindi ataingia fainali Jumamosi.
Upande wa wanaume nao hawakuwa nyuma. Wameshinda dhidi ya Singapore, Bangladesh, Scotland na Canada.
Mechi iliyovutia ni dhidi ya Bangladesh Oktoba 25, ambapo Kenya ilishinda kwa alama 32-31 pointi moja tu!
Nyota wa wanaume pia wameangaza. Nahodha James Kamweti alitajwa Best Raider na Lewis Maviri Best Defender dhidi ya Scotland. Makamu nahodha Stephen Amollo na Reuben Mburu wakapata tuzo za Best Raider na Best Defender dhidi ya Canada.
Chini ya Kamweti na Amollo, wanaume watamenyana na Sri Lanka
leo kutafuta tiketi ya fainali.
Mchezo huu uliletwa Kenya na Bi Laventer Oguta aliyeugundua kupitia video za mtandaoni na kuanza kuufundisha jijini Nairobi.
Akiwa na Bw Silas Jakakimba, viongozi hao wawili ndio waasisi waliopigania mchezo huu ukue na kutambulika nchini.
Kutoka Nairobi, sasa Kabaddi imeenea katika kaunti zote 47, ikipa vijana nafasi ya kushiriki mashindano.
Kwa miaka hii, Kenya imejijenga kama taifa namba moja barani Afrika. Mafanikio yake ni pamoja na kutwaa ubingwa wa Afrika mara nne, medali ya shaba Kombe la Dunia la Ufukweni kwa Wanaume, fedha Kombe la Dunia la Vijana, fedha mara mbili Kombe Bangabandhu na nafasi ya tano Kombe la Dunia la Wanawake.
Mafanikio ya Ahmedabad ni matunda ya zaidi ya muongo mmoja wa kujitolea, kukuza vipaji mashinani, mashindano ya nyumbani na uwakilishi wa kimataifa.
Shirikisho la Kabaddi Kenya (KKU) limeimarisha miundo yake, ikiwemo Ligi Kuu ya Kabaddi ya Kenya, ambayo ndiyo chachu ya kupata wachezaji wa timu za taifa.