HabariSiasa

Waliopatanisha Uhuru na Ruto wakanusha maagano ya urithi 2022

March 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JUSTUS OCHIENG

WANASIASA waliohusika katika kuwaleta Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto pamoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2013, wamekanusha kulikuwa na maafikiano ya Naibu Rais kurithi urais 2022.

Maafisa wa vyama vilivyovunjwa vya The National Alliance (TNA) na United Republican Party (URP), wamefichua kuwa maelewano yaliyokuwepo yalihusu kipindi cha kwanza cha utawala wao hadi 2017.

Wakati huo Rais Kenyatta alikuwa kiongozi wa TNA naye Dkt Ruto akiwa kinara wa URP.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa TNA, Bw Onyango Oloo (pichani juu), ambaye pamoja na mwenzake wa URP, Bw Davis Chirchir na maafisa wengine kama vile Johnson Sakaja (Mwenyekiti, TNA) na Francis ole Kaparo (Mwenyekiti, URP) walikuwa na majukumu muhimu katika makubaliano hayo.

“Nilikuwa Katibu Mkuu wa TNA na bado ninakumbuka vyema. Mkataba tuliopeleka kwa msajili wa vyama vya kisiasa ulistahili kudumu kwa miaka mitano,” akasema Bw Oloo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kisheria wakati Chama cha Jubilee kilipoundwa Septemba 2016.

“Mkataba ulisema kama tungeshinda, Uhuru angekuwa Rais na Ruto Naibu Rais, na serikali itaundwa kwa kugawana madaraka kwa nusu. La muhimu zaidi kwenye maelewano hayo, ambayo nilitia sahihi pamoja na wenzangu watatu, ni kwamba hapakuwa na sehemu yoyote iliyosema Uhuru angehudumu kwa miaka mitano au kumi, kisha ampishe William Ruto kuongoza kwa miaka mingine mitano au kumi,” akasema.

Aliongoza: “Hayo ni maoni ya wanasiasa ambao wanaamini wana haki kurithi urais kutoka kwa Uhuru.”

Bw Oloo aliema ushirikiano wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto ulionekana kama njia muhimu ya kuwawezesha kupata mamlaka ya kisiasa, ili iwasaidie kukabiliana na kesi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kwa upande wake, Bw Kaparo pia alisema hapakuwa na maelewano kwamba Rais atamkabidhi mamlaka naibu wake: “Sidhani kulikuwa na maelewano kama hayo. Lakini hata tukisema yalikuwepo, hivyo vilikuwa vyama viwili tofauti, URP na TNA, ambavyo sasa havipo,” akasema Bw Kaparo.

Bw Chirchir na Bw Sakaja, ambaye sasa ni Seneta wa Nairobi, hawakujibu kuhusu makubaliano hayo ya 2012 walipotafutwa.