• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Bao tamu la Wanyama lapigiwa upatu kuibuka goli bora la Februari EPL

Bao tamu la Wanyama lapigiwa upatu kuibuka goli bora la Februari EPL

Na GEOFFREY ANENE

KIKI zito alilofunga kiungo Mkenya Victor Wanyama wakati klabu yake ya Tottenham Hotspur ililazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield limo mbioni kutawazwa goli bora la mwezi wa Februari.

Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti kwamba bao la Wanyama, ambalo lilipatikana aliposukuma kombora kali wavuni kutoka nje ya kisanduku Februari 4, linawania tuzo hiyo dhidi ya lile kutoka kwa mwanasoka bora wa Afrika Mohamed Salah (Liverpool) na bao ambalo Sergio Aguero alifungia Manchester City ilipobwaga Leicester City 5-1 Februari 10.

Wachezaji wengine ambao mabao yao pia yanawania tuzo hiyo ni Jose Izquierdo wa Brighton & Hove Albion dhidi ya Stoke na dhidi ya West Ham, Adam Smith wa Bournemouth dhidi ya Newcastle United na Mario Lemina wa Southampton dhidi ya West Bromwich Albion.

Nahodha wa Keya, Wanyama, aliingia mchuano wa Liverpool katika dakika ya 79 akijaza nafasi ya Mousa Dembele. Kabla hata ya wino kukauka, Wanyama aliona lango kupitia shuti kali dakika ya 80 akisawazishia Spurs 1-1.

Salah aliweka Liverpool bao 1-0 juu dakika ya tatu kabla ya Wanyama kusawazisha. Mvamizi matata Harry Kane alikosa nafasi ya kuweka Spurs mabao 2-1 mbele alipopoteza penalti dakika ya 87 kabla ya Salah kupachika bao tamu dakika ya 91 ambalo linawania tuzo ya goli bora la Februari. Kane alipata nafasi nyingine ya kufuma penalti dakika ya 95 na hakukosea, mechi hiyo ikamalizika 2-2.

You can share this post!

Ndoto ya Birgen kushindia Kenya medali yatimia

Shujaa kumenyana na Fiji na Ufaransa tena

adminleo