• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KINAYA: Sitaki kumeza mate, ninataka kula nyama tuliyosaidiana kunasa 2013

KINAYA: Sitaki kumeza mate, ninataka kula nyama tuliyosaidiana kunasa 2013

Na DOUGLAS MUTUA

NIMEONA chui!

Nimemsikia Tuju! Nimemsikia Nyanja pia! Hizo ni sauti zao kabisa. Wapi? Subiri kidogo, nitakueleza.

Nimeona wengine wanaotaka kuniua ili nisiwe Rais.

Wamekuwa wakikutana usiku hotelini ili kula njama ya kuniangamiza!

Hotelini, kwa sababu hawana nyumba zao binafsi wanamoweza kukutana na kupanga maovu hayo.

Labda wana nyumba, lakini ni mazuzu kiasi kwamba hawajui siku hizi hata anayekuuzia chai mkahawani unakokwenda ni kachero wangu.

Wajua, kila mtu katika nchi hii anataka niwe Rais ifikapo 2022.

Nimesema kila mtu kwa sababu hao wachache wanaonipinga si watu. Mtu kamili akili, tusizoeane.

Kumbuka hao wanaotaka kuniua ni wafanyakazi wangu wanaopaswa kuwa waaminifu kila wakati badala ya kutaka kuniondoa duniani.

Acha kiherehere bwana, sioti mchana wa jua la utosi.

Hao ni wafanyakazi wangu kwa sababu nina ubia wa kisiasa na ndugu yangu kutoka kijiji cha Ichaweri.

Kumbuka mimi naye tuliingia msituni tukawinda kwa bidii, mwisho wa siku tukamfuma mishale na kumwangusha swara mnono mnamo 2013.

Ni baada ya kumwangusha swara huyo ambapo mimi na ndugu yangu tuliamua ni nani wa kupewa kisu awakatie Wakenya nyama ili washibe.

Minofu iende wapi?

Kazi yetu ilipaswa kuwa rahisi: kuwaelekeza wafanyakazi wetu hao kwa kupeleka minofu minono ya nyama, wapi kwa kwenda mifupa na hata harufu pekee.

Sasa nimejua sijui! Kumbe vile visu virefu vyenye makali ya kutisha havikuwa vya kukata nyama pekee?

Hivi mtu anawezaje kuota visu hivyo vikiniingia tumboni? Si kichaa hicho?

Wewe mfanyakazi wako akikutishia kwa kisu unamfuta kazi au unamwitia polisi?

Hilo ni swali ambalo limenizuga akili kwelikweli, lakini nadhani muhimu ni kuikadiria hatari.

Najua wewe na papara zako utasema kwanza nimpige kalamu mfanyakazi wa aina hiyo, eti tuongee mambo haya naye akiwa nje ya lango langu.

Mambo si rahisi hivyo; ninahitajika kujadiliana na ndugu yangu ili nimshawishi kuamini kwamba kwa hakika visu si vya nyama tena, vinaniwinda.

Usinione mwoga mkuu zaidi nchini humu; labda nimejaribu kumwelewesha ndugu yangu akanicheka akidhani mimi ni kikojozi.

Nielewe, mimi si mwoga. Nilivumilia kung’atwa na mbu na mbung’o nilipokuwa nikichunga mifugo ya babangu, naye ndugu yangu akilala chini ya chandarua cha mbu Ikulu.

Usinione hivyo, nimetoka mbali sana.

Kwa kweli mahali nilitoka saa hizi hapapitiki. Hapakaliki. Ukiona nikiwapigia polisi simu kuwashtaki wafanyakazi wangu, nimekwama.

Mimi ni mnyonge mbele ya ndugu yangu, sina mamlaka, sina uwezo.

Hata kama kikatiba hawezi kunitimua, mimi ndimi dhaifu zaidi. Siwezi kumfuta yeyote kazi.

Hata basi nililosaidia kukarabati ili hatimaye niliabiri katika safari yangu ya kuelekea Ikulu linaendeshwa na dereva mang’aa na mkora! Hanitambui. Haniheshimu. Hanitaki.

Hivi hawa watu wote wametumwa na nani? Nimefanya makosa gani kwa kuonyesha niko radhi kupokea malipo ya madeni yangu ya 2013 na 2017 watu wakiamua kunilipa?

Sijamkosea yeyote, hata ndugu yangu anajua hivyo.

Wanakijiji wa kwao ambao amezomea juzi kwa kutomtii pia hawana makosa kunifuatafuata, wanatafuta kazi jamani.

Kila mmoja anatamani nimchukue awe msaidizi wangu ili nikiwa mgavi mkuu wa swara hapo 2022 asilale njaa.

Sote hatutaki kumeza mate; tunataka kula nyama.

[email protected]

You can share this post!

Mume mchafu afungiwa bafuni aoge

Kamket apuuza madai ya njama ya kumuua Ruto

adminleo