Habari

Majaji wapya wateuliwa ICC kusikiza kesi za Uhuru na Ruto zikifufuliwa

March 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) imechagua majaji wapya kusimamia kesi za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, Bw William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, iwapo Kiongozi wa Mashtaka wa korti hiyo ataamua kuzifufua.

Ingawa kesi hizo zilisitishwa kufuatia ukosefu wa ushahidi wa kutosha, Kiongozi wa Mashtaka, Bi Fatou Bensouda, aliambiwa yuko huru kuzifufua endapo atafanikiwa kukusanya ushahidi mpya.

Mwishoni mwa 2017, ilifichuka wapelelezi wa ICC walikuwa nchini Kenya kuchunguza masuala yanayohusiana na kesi ya Bw Ruto ambaye alishtakiwa pamoja na mtangazaji wa zamani wa redio, Bw Joshua Sang.

Ufichuzi huo ulitolewa kupitia kwa ripoti ya kila mwaka kuhusu shughuli za afisi ya upande wa mashtaka.

Mahakama hiyo Jumamosi ilifanya mabadiliko ya majaji baada ya majaji sita wapya kuchaguliwa wiki mbili zilizopita huku wengine waliokuwepo wakipewa majukumu mapya na baadhi yao kukamilisha muda wao wa kuhudumu.

Jaji Chile Eboe-Osuji ambaye wiki iliyopita alichaguliwa kuwa rais wa ICC, sasa atakuwa akihudumu kwenye kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo. Awali, alikuwa Jaji Msimamizi wa kesi ya Mabw Ruto na Sang.

Kesi hiyo sasa itaendeshwa na Majaji Robert Fremr, Reine Alapini-Gansou na Kimberly Prost, ambao pia wataendesha kesi dhidi ya Rais Kenyatta.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, mahakama hiyo jana ilisema mabadiliko hayo ambayo yameathiri kesi karibu zote zilizo mbele yake yamechukuliwa ili kuboresha utoaji huduma.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa afisi ya rais wa ICC ilizingatia uwezo na weledi wa majaji katika sheria za uhalifu wa kimataifa wakati mabadiliko hayo yalipofanywa.

“Majaji watahudumu kwa miaka mitatu, na baadaye hadi wakati kesi zitakapokamilika,” ikasema taarifa hiyo.

Kufuatia hatua hii, vyumba vya mahakama vya Tano (A) na Tano (B) ambavyo vilikuwa vikutumika kusikiliza kesi ya Bw Ruto na Rais Kenyatta mtawalia vilivunjiliwa mbali.

Kesi zote za Wakenya sita waliodaiwa kuhusika pakubaa zaidi na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilisitishwa baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuhusika kwao.

Bi Bensouda alilalamika kuwa uamuzi wake kusitisha kesi za Rais Kenyatta, Bw Ruto na Bw Sanga ulitokana na kuwa mashahidi walishawishiwa kujiondoa ambapo baadhi walitishiwa maisha yao, wengine wakauawa na wengine wakatoweka katika hali ya kutatanisha.

Alidai pia serikali ya Kenya ilikataa kumsaidia kukusanya ushahidi aliohitaji ilhali serikali ina jukumu hilo kwani taifa hili ni mwanachama wa ICC kupitia uratibishaji wa Mkataba wa Roma ambao ndio msingi wa sheria za mahakama hiyo iliyo The Hague, Uholanzi.

Hata hivyo, madai haya yalikanushwa na serikali ambayo iliwakilishwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Prof Githu Muigai.