PATA USHAURI WA DKT FLO: Makamasi kooni yazima starehe
Na DKT FLO
Mpendwa Daktari,
NINGEPENDA kukueleza kuhusu tatizo na ukosefu wa starehe ninaoshuhudia kwa sababu ya kutokwa na kamasi kooni mwangu. Nimekuwa nikikumbwa na hali hii kwa muda sasa. Nimetafuta ushauri kutoka kwa wataalamu kadha wa ENT katika hospitali za haiba ya juu, lakini bado sijapata utulivu. Kamasi hii huwa nzito asubuhi na tatizo hili huzidi baada ya kula chakula chenye sukari, nikiwa na mafua au baada ya kunusa kitu chenye harufu kali. Sina uchungu wala hakuna chembechembe za damu kwenye kikohozi. Ningependa kujua tatizo ni lipi?
David
Mpendwa David,
Kwa kawaida mkondo unaopitisha hewa hutoa kamasi. Kila unapokumbwa na tatizo kutokana na baridi, vumbi, harufu kali, chavua au maambukizi, kiwango cha kamasi huongezeka na mwili hujaribu kuyaondoa kupitia kukohoa au kuchefua. Iwapo kuna maambukizi, tiba itasaidia mwili kurejelea hali yake ya kawaida. Kuna baadhi ya watu ambao hutoa kamasi nyingi kutokana na sababu kwamba mfumo wao wa kinga una shughuli nyingi sana, au waishipo pana vumbi na vitu vingine vinavyochochea mwasho. Wakati mwingine hata asidi inayorejea kutoka tumboni hadi kooni (stomach acid reflux) yaweza kusababisha kuzalishwa kwa kamasi. Na kuondoa kikohozi kooni kwa kukohoa kila mara, husababisha mwasho na kusababisha uzalishaji zaidi wa kamasi. Unapaswa kutambua na kuondoa chochote kinachosababisha mwasho kwa mfano kuepuka baridi. Mfumo wa kinga hauwezi kubadilishwa, lakini waweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa za kukabiliana na mzio inapohitajika. Aidha, ni jambo la busara kufanyiwa uchunguzi wa kila mara na mtaalamu wa ENT.
******
Hujambo, nina umri wa miaka 28. Kwa miaka kumi sasa, uzani wangu umekuwa kati ya kilo 68 na 70 na kimo changu ni sentimita 180. Nina hamu kubwa ya chakula na hata nimekuwa nikitumia vijalizo vya vyakula (supplement foods). Nimefanyiwa chunguzi kadha kubaini ikiwa nina maradhi yoyote, lakini zote zinaonyesha kwamba sina tatizo. Nina wasiwasi. Nifanye nini kuongeza mafuta mwilini? Tafadhali nisaidie.
Steve
Mpendwa Steve,
Kimo cha sentimita 180 na uzani wa kati ya kilo 68 na 70 yaonyesha kwamba una afya. Kimo chako kikilinganishwa na uzani wako (BMI) ni 21 (BMI ya kawaida ni kati ya 18 na 25). Japo kuna baadhi ya watu wanaoongeza uzani upesi, wengine hawabadilishi uzani kwa urahisi. Ni afya nzuri kuwa na uzani usiobadilika sana. Unapozidi kukomaa kiumri, itakuwa rahisi kuongeza uzani kwani mfumo wa umetaboli utakuwa chini. Dhana kwamba unene ni ishara ya afya njema ni potovu. Ikiwa uzani wako ni thabiti na uko katika kiwango sawa cha afya, na haukumbwi na matatizo ya kiafya kama vile kushambuliwa na maradhi upesi, basi haupaswi kuwa na wasiwasi. Zingatia lishe yenye afya, fanya mazoezi na ujiepushe na tabia zinazokuweka kwenye hatari kiafya, kama vile kuvuta sigara au kunywa pombe kupindukia. Unapaswa kuukubali mwili wako jinsi ulivyo kwani uko sawa.
******
Mpendwa Daktari,
Nina tatizo la mba. Nimejaribu aina nyingi za mafuta bila mafanikio. Je, kuna suluhisho kwa tatizo hili?
Asante.
Emma
Mpendwa Emma,
Mba ambazo pia zinafahamika kama seborrheic dermatitis, ni tatizo la ngozi linalosababisha mwasho na chembechembe za magamba. Kwa kawaida huathiri ngozi ya kichwa, lakini pia yaweza kuathiri sehemu zingine za mwili. Kiini chake hakijulikani, lakini pia yaweza kutokana na mawazo mengi, ngozi yenye mafuta mengi, au maambukizi ya kuvu, vile vile baridi. Kuna baadhi ya matatizo ya kiafya na dawa ambayo pia yaweza kuchochea shida hii. Mambo huwa mabaya na kuimarika baada ya muda. Unaweza kutumia shampuu au krimu kama vile ketoconazole selenium, zinc au salycilic acid. Kwa kawaida dawa hizi zinauzwa katika maduka ya dawa au zaweza pendekezwa na daktari. Pia, kunywa maji mengi na uhakikishe lishe bora. Jaribu usijikune kichwani kwani hii yaweza kusababisha maambukizi. Iwapo tatizo hili litaendelea licha ya kutumia dawa hizi, tafuta ushauri kutoka kwa mtaalamu wa ngozi (dermatologist).