Marafiki walienda wapi?
Na PAUL WAFULA
WATU walioshikilia nyadhifa za juu serikalini kabla ya kuondolewa kwa sababu kadhaa ikiwemo ufisadi, wameeleza jinsi walivyotengwa na marafiki na sasa wanaishi maisha ya upweke.
Simu zao sasa hazilii mara nyingi kama ilivyokuwa zamani. Baadhi ya marafiki wao wamewatoroka na wengine wanahisi kusalitiwa naserikali ambayo walitumikia majina yao yalipoibuka kwenye orodha ya washukiwa wa ufisadi.
Na wanapowaalika marafiki wao wa zamani kwa hafla mbalimbali manyumbani mwao, ni wachache huitikia mwaliko huo tofauti na awali hafla zao zilipokuwa zikifurika watu.
Aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Ugatuzi, Peter Mangiti, juzi alisimulia Taifa Leo mengi kuhusu maisha yake ya upweke baada ya kuondolewa afisini kwa tuhuma za ufisadi.
Mhandisi Mangiti alishtakiwa kuhusiana na sakata katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) iliyohusisha Sh791 milioni.
“Nimejifunza mengi ndani ya miaka minne baada ya kufutwa kazi kuliko yale ambayo nimejifunza katika miaka yangu yote ya utu uzima,”
alisema tulipokutana naye katika uwanja wa mchezo wa gofu wa Royal Golf Course, ulioko kando ya barabara ya Ngong Road, juzi.
Wakati hayuko kortini kuhudhuria kesi dhidi yake, Mangiti hutumia wakati wake akicheza gofu katika uwanja huo ili kujiondolea baridi na upweke.
Lakini mara nyingi, yeye hujipata akicheza pekee yake tofauti na zamani ambapo marafiki wengi wangeungana naye. Hata hivyo, anasema hana kinyongo na mtu yeyote.
“Mzigo wa usaliti unawalemea marafiki zangu walionitoroka baada ya kusikia nilikuwa mashakani, wala sio mimi,” Bw Mangiti anasema.
Anaongeza: “Hata hivyo, kwa upande mwingine, upweke huu umekuwa baraka kwangu. Umeniwezesha kuwafahamu marafiki feki na wale halali.”
Mangiti anakubali kuwa maisha nje ya afisi na mamlaka, yamekuwa magumu. Alikuwa na magari matatu lakini akalazimika kuuza mawili na kusalia na moja pekee. Likipata hitilafu analazimika kutumia teksi ya Uber au matatu.
“Hebu fikiria kwamba nilikuwa nikipokea mshahara wa Sh1 milioni kwa mwezi. Lakini sasa napata Sh68,000 pekee. Maisha ni magumu.
Lakini sina machungu. Ikiwa unapitia changamoto kama hizi ukiongeza hasira, unaweza kufa kwa haraka,” alisema.
Lakini tofauti na makatibu wa wizara wa zamani na magavana ambao kesi zao zimeanza juzi, Dkt Mangiti amefaulu kushinda kesi moja iliyomkabili. Ni mwingi wa matumaini kuwa atashinda kesi zingine na kufurahia uhuru wake kwa ukamilifu.
Naye aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero, alikuwa mtu mwenye marafiki wengi. Mambo yalipokuwa mazuri kwake, angetembelewa na watu mashuhuri katika makazi yake ya kifahari.
Na kwa mara kadhaa, Rais Uhuru Kenyatta angemtembelea afisini mwake. Alikuwa miongoni mwa magavana wachache ambao walikubalika na mirengo yote ya kisiasa.
Na alipofikishwa kortini akiwa mamlakani kama gavana, wafuasi wake walikuwa kando yake wakimtetea na hata kufurika kortini. Lakini baada ya kuondoka afisini na kuandamwa na kesi za ufisadi, marafiki wa Dkt Kidero wamepungua.
Siku hizi, yeye huonekana pekee yake kortini au kwenye viwanja vya gofu ambavyo hupenda kuvinjari.
Wanasiasa ambao zamani walikuwa wakipiga foleni afisini mwake wakitafuta usaidizi wa kifedha kwa ajili ya michango mbalimbali ya harambee wamemuambaa kama jini.
Dkt Kidero amekuwa akiandamwa kila mara na wapelelezi na kufungiwa katika seli za polisi mara kadhaa.
Wakati huu, Dkt Kidero anapambana na kesi mbili mahakamani za kuamuru malipo ya Sh217 milioni na Sh68 milioni kwa kampuni kadhaa kinyume cha sheria.
Kazungu Kambi
Waziri wa zamani Bw Kazungu Kambi ni mmoja wa mawaziri watano waliopigwa kalamu kwa tuhuma za ufisadi mnamo 2015.
Wakati huo alikuwa akihudumu kama Waziri wa Leba.
Lakini sasa anasema amesahau madhila yaliyompata na kuamua kupatia maisha sura mpya. Hata hivyo, anasema kuwa aliivumilia maisha ya upweke kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja uchunguzi dhidi yake ulipokuwa ukiendelea.
Baada ya kuondolewa lawama aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ustawi wa eneo la Pwani (CDA).
Isitoshe, Waziri wa Fedha Henry Rotich na Katibu wake Kamau Thugge ni maafisa wa kwanza nchini Kenya, katika vyeo hivyo, kusukumwa kortini kwa mashtaka ya ufisadi.
Kwa muda wa mwezi mmoja uliopita, hatujaweza kumpata Bw Rotich kuongea nasi kuhusu maisha yake nje ya afisi hiyo yenye hadhi na mamlaka ya juu
Wiki jana, alituambia kwamba alikuwa amesafiri mashambani kwa shughuli za kibinafsi.
Dkt Thugge hakuwa anajulikana zaidi kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Wizara ya Fedha mnamo 2010. Hii ni kwa sababu alizama katika ulimwengu wa usomi kisha akaajiriwa katika Shirika la Kifedha Ulimwenguni (IMF).
Kukamatwa kwake kulimshtua ikizingatiwa kuwa hajawahi kuhusishwa katika sakata yoyote ya ufisadi maishani mwake.
Alipokuwa akihudumu, alikuwa akiishi katika makazi ya kifahari ya Norfok Apartments kilomita chache kutoka afisi yake.