Walanguzi wa mihadarati sasa wageukia mita za maji
NA KALUME KAZUNGU
BODI ya Usimamizi na Usambazaji wa Maji Katika Kaunti ya Lamu (LAWASCO) inahofia kupoteza mamilioni ya fedha kufuatia ongezeko la uharibifu wa mita za maji ambazo zinalengwa na walanguzi wa dawa za kulevya.
Ufichuzi umebaini kuwa waraibu wa mihadarati katika kisiwa cha Lamu wamezindua mbinu mpya ya kukimu kiu yao ya dawa za kulevya, ambapo wamekuwa wakigeukia mita za maji na kuzibomoa ili kutoa poda ambayo ni kemikali maalum inayotumiwa kuhifadhia mita hizo zisiharibike.
Poda hiyo baadaye huvutwa na pia kuliwa na walanguzi hao wa dawa ambao kisha hulewa chakari.
Akizungumza na wanahabari mjini Lamu Jumatano, Mwenyekiti wa Bodi ya Maji (LAWASCO), Bw Mohamed Athman, alisema zaidi ya mita 350 za maji ambazo zinagharimu kima cha takriban Sh 2.1 milioni tayari zimeharibiwa na walanguzi hao wa dawa za kulevya katika harakati zao za kutafuta kemikali ya kuwalewesha.
Bw Athman alitaja mitaa ya Langoni, Mkomani, Gadeni, Bajuri na Kashmir kuathirika zaidi na visa hivyo vya mita za maji kulengwa na walanguzi.
“Visa zaidi ya 350 vya mita za maji kuharibiwa na walanguzi wa dawa za kulevya vimeripotiwa katika afisi yetu. Waraibu wa mihadarati wanavunja mita na kutoa unga ambao ni kemikali maalum inayowekwa ndani ya mita hizo ili kuzihifadhi zisishike kutu au kuharibika.
Tumegundua kuwa kemikali hiyo ndiyo inayotafutwa na walanguzi wa dawa kwa minajili ya kuivuta au kuiramba. Baadaye wao hulewa chakari kushinda dawa nyingine zozote za kulevya,” akasema Bw Athman.
Naye Meneja wa LAWASCO, Bw Paul Maina, alisema visa hivyo vimechangia kupotezwa kwa bili za maji zinazotumiwa kwenye majumba tofauti tofauti mjini Lamu na kisha mwishowe mita zao za maji kuharibiwa na waraibu wa dawa za kulevya.
Bw Maina alisema tayari wametoa tangazo kwa wamiliki wa mita za maji majumbani mwao kuzitunza ili zisiharibiwe na walanguzi hao wa dawa za kulevya.
“Mita zinazoharibiwa ndizo zinazotuwezesha kusoma bili za maji zinazotumika majumbani. Mita hizo zinapoharibiwa kabla ya bili kusomwa, itamaanisha ushuru unaotozwa kwa matumizi ya maji hayo unapotea.
Ningewasihi wenye mita hizo kuwa makini ili zisiharibiwe. Pia itakuwa bora iwapo wanaojenga nyumba watazingatia kuziweka mita hizo ndani ya nyumba zao ili zisifikiwe na waharibifu,” akasema Bw Maina.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na Taifa Leo aidha walieleza hofu yao kuhusiana na kemikali mpya inayotumiwa na vijana kulewa.
Bw Ahmed Omar Bingwa, aliitaka idara ya usalama ya kaunti ya Lamu kuwa macho na kuwakamata wale watakopatikana wakivunja mita za maji ili kutoa kemikali hiyo.
“Tushirikiane sisi wakazi na kuwasema hadharani wale wanaopatikana wakivunja hizo mita za maji. Kemikali yenyewe ni hatari. Vijana wetu wakiendelea kutumia poda hiyo wataharibika hata zaidi. Idara ya usalama iangazie tatizo hilo na kulikomesha,” akasema Bw Bingwa.