Msako dhidi ya Al-Shabaab msituni Boni waanzishwa
NA KALUME KAZUNGU
MAAFISA wa usalama kwen-ye msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu wameanzisha msako mkali dhidi ya magaidi wa Al-Shabaab waliojaribu kuvamia kambi ya polisi wa kushika doria mpakani (RBPU) mnamo Jumanne.
Wakati wa uvamizi huo uliotekelezwa majira ya saa nane unusu alfajiri, magaidi wapatao 20 wa Al-Shabaab waliokuwa wamejihami kwa silaha hatari walivamia kambi hiyo ya RBPU iliyoko eneo la Mangai na kuanza kufyatua risasi kila upande.
Maafisa waliokuwa kambini walijibu, hivyo ufyatulianaji mkali wa risasi ukazuka kati ya magaidi na polisi na kudumu kwa zaidi ya robo saa.
Akizungumza na Taifa Leo Jumatano asubuhi, Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi ambaye pia ni Kamanda wa Operesheni ya Linda Boni, Douglas Kirocho, alisema afisa mmoja wa polisi alijeruhiwa begani wakati wa makabiliano hayo.
Bw Kirocho alisema baadaye magaidi walishindwa nguvu na kutorokea kwenye msitu wa Boni.
“Ilikuwa yapata majira ya saa nane unusu asubuhi ambapo magaidi wa Al-Shabaab walivamia kambi ya RBPU ya Mangai na kuanza kufyatua risasi kila upande.
Maafisa wetu walijibu mara moja na kuwashinda nguvu magaidi hao waliotokomea kwenye msitu wa Boni. Mmoja wa maafisa wetu wa polisi alijeruhiwa begani na tayari amesafirishwa kwa ndege kwa matibabu ya dharura,” akasema Bw Kirocho.
Shambulizi hilo pia lilithibitishwa na Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Lamu Mashariki, Gideon Mugambi aliyesema usalama umeimarishwa vilivyo kwenye eneo husika na hata sehemu zingine zinazokaribiana na msitu wa Boni.
Alisema shughuli ya kuwatafuta waliotekeleza shambulizi hilo pia inaendelea kwa sasa.
Aliwataka wakazi eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama na kupiga ripoti iwapo watashuhudia tukio au mtu yeyote wanayemshuku kuwa kero kwa usalama wa taifa.
“Maafisa wa usalama ni wengi kabisa ndani ya msitu wa Boni na maeneo yanayokaribiana. Ningewasihi wananchi kuwa macho na kutupasha ripoti iwapo watashuhudia wahalifu wakikaribia maeneo yao,” akasema Bw Mugambi.