Habari Mseto

Hospitali yakataa kuachilia maiti ikazikwe

April 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na SHABAN MAKOKHA

FAMILIA moja katika eneo la Lurambi kaunti ya Kakamega inaomba msaada wa zaidi ya Sh2.3 milioni kulipia gharama za matibabu ya hospitali na ada ya mochari ndipo ikubaliwe kuchukua mwili wa jamaa yao na kuuzika.

Mwili wa Vincent Khashiya unazuiliwa katika hospitali moja mjini Eldoret.

Hospitali hiyo imekataa kuruhusu familia ya Khashiya kuchukua maiti yake hadi pale gharama za hospitali zitakapolipwa.

Familia ya marehemu imeshindwa kabisa kupata pesa za kulipa hospitali hiyo.

Mjane wa marehemu Bi Vivian Mwandi ametoa wito kwa Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega, Seneta Cleophas Malala, Mbunge wa Lurambi Bw Titus Khamala kuwasaidia kulipa gharama za hospitali na za Mochari.

Khashiya alilazwa katika hospitalini mnamo Februari 10.

Aliaga dunia baada ya wiki mbili akiendelea kupokea matibabu ya Saratani ya damu.

Mama yake mwendazake Bi Margaret Ingato alisema kila juhudi imefanywa kupata pesa hizo lakini mambo yamegonga mwamba.

Gharama ya hospitali ni Sh2.3 milioni nayo ada ya mochari ni Sh50,0000.

Bi Ingato alisema hospitali inawataka walipe Sh1.5 milioni pesa tasilimu kisha wawasilishe hati ya umiliki wa shamba ama kitabu cha umiliki wa gari ndipo wakubaliwe kuondoa mwili wakauzike.

Hazina ya kitaifa ya bima ya afya (NHIF) imewalipia Sh200,000.