• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Karua ataka korti iagize upya vifaa vya kura Kirinyaga vikaguliwe

Karua ataka korti iagize upya vifaa vya kura Kirinyaga vikaguliwe

Na JOSEPH WANGUI

KIONGOZI wa Chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua, anataka maagizo mapya ya korti kuhusu ukaguzi wa vifaa vya uchaguzi vilivyotumiwa kwenye uchaguzi wa gavana katika Kaunti ya Kirinyaga mnamo Agosti 8, 2017.

Kulingana na Bi Karua, ombi lake limetokana na kuwa maagizo ya awali ya mahakama hayakutimizwa.

Alisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikataa kutimiza maagizo ya mahakama yaliyotolewa Oktoba 23, 2017, kukagua vifaa hivyo.

Huku akitoa ushahidi kwenye kesi aliyowasilisha kupinga ushindi wa Gavana Anne Waiguru, waziri huyo wa zamani wa haki na masuala ya kikatiba alisema uchaguzi ulikumbwa na makosa na ukiukaji wa sheria ikiwemo kuongezwa kwa kura za Bi Waiguru kiharamu.

“Ukaguzi ulifanywa katika Jumba la Anniversary na tume ilikataa au ilipuuza kutimiza maagizo ya mahakama.

Vifaa vyote vya kusimamia uchaguzi kielektroniki (KIEMS) havikuletwa na hatukuweza kusoma yaliyokuwemo kwenye vifaa hivyo,” akasema Bi Karua, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Lucy Gitari.

Zaidi ya hayo, aliambia mahakama kwamba yeye pamoja na wakili wake Gitobu Imanyara, hawakupewa kadi za kuhifadhi habari ambazo zilitumiwa kwenye vifaa hivyo.

Aliongeza kwamba kufuatia makosa yaliyotendwa wakati wa uchaguzi ikiwemo uhongaji wa wapigakura, aliandika barua kwa afisa wa kusimamia uchaguzi katika kaunti na katika eneobunge la Mwea kutaka kura za ugavana zihesabiwe upya.

Mahakama iliambiwa kuwa afisa wa IEBC, Seki Lempaka, alikataa kuhesabu kura upya na kusema ni mahakama pekee inayoweza kumwagiza kufanya hivyo.

“Wagombeaji wana haki ya kuhesabiwa kura mara mbili. Kukataa kwake kulikuwa ni ukiukaji wa haki hizo,” akasema.

Hata hivyo, Bi Karua alipata pigo wakati jaji alipomzuia kuwasilisha ushahidi zaidi katika kezi hiyo.

“Utatanishi ni kuwa ripoti ya mlalamishi si kile kilichotumwa na msajili wa mahakama kwa wahusika wa kesi hii. Washtakiwa wamesema watakubali ripoti ya msajili pekee,” akasema Jaji Gitari.

Kesi hiyo itaendelea Mei 2, wakati Bi Karua atakapowasilisha video anayodai inaonyesha matukio ambapo sheria za uchaguzi zilikiukwa.

Anatarajiwa pia kuwasilisha mukhtasari wa ripoti ya fomu za uchaguzi na baadaye atahojiwa na mawakili wa Bi Waiguru.

You can share this post!

Kongamano la Ugatuzi: Wajumbe wakerwa na kujikokota kwa...

Waliojaribu kuuzia polisi pembe huru kwa bondi ya Sh1m

adminleo