Habari Mseto

Wanajeshi wawili na polisi wauguza majeraha baada ya kushambuliana kimakosa

May 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

WANAJESHI wawili kutoka kikosi cha Kenya (KDF) na polisi mmoja wanaendelea kuuguza majeraha waliyopata baada ya kufyatuliana risasi eneo la Bura Mashariki, kaunti ndogo ya Fafi, Garissa.

Maafisa hao wamejipata katika mkasa huo baada ya kila moja ya pande hizi kudhani upande mwingine ni wa magaidi.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi eneo la Fafi, George Sangalo amesema kulikuwa na hali ya mkanganyiko kati ya vikosi maalum.

“Lilikuwa kosa. Helikopta iliyokuwa na maafisa kutoka Nairobi ilikuwa inaelekea Bura Mashariki huko Fafi,” amesema Sangalo.

Taarifa ya polisi ambayo Taifa Leo imeona inasema kwamba afisa mmoja wa polisi na wanajeshi wawili walipata majeraha baada ya kumiminiana risasi kimakosa.

“Konstebo wa polisi alimiminiwa risasi na wanajeshi wawili wa KDF naye akiwashuku kwamba maafisa hao ni wapiganaji wa kundi la kigaidi, aliwapiga risasi na kuwajeruhi vibaya,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Afisa huyo wa polisi alikuwa akitembea kwa miguu akitoka katika nyumba moja eneo la mji huo.