• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Mwanajeshi na polisi waliofyatuliana risasi kimakosa wafariki

Mwanajeshi na polisi waliofyatuliana risasi kimakosa wafariki

Na FARHIYA HUSSEIN

MWANAJESHI na polisi waliopata majeraha kwa kufyatuliana risasi kimakosa wamefariki kutokana na majeraha waliyopata Bura Mashariki, Fafi, Kaunti ya Garissa.

Konstebo Emmanuel Ngao na afisa wa KDF David Mbugua walikuwa wamewahiwa katika Hospitali ya Bura na baadaye wakafariki na miili yao kusafirishwa hadi mochari katika Kaunti ya Nairobi.

“Miili miwili; mmoja wa afisa wa polisi na mwingine wa mwanajeshi imesafirishwa Chiromo na Forces Memorial, Nairobi na kwamba itafanyiwa upasuaji,” inasema ripoti ya polisi.

Kabla ya kufariki, wawili hao na mwanajeshi mwingine Jeremy Malusi walipata majeraha baada ya kufyatuliana risasi eneo la Bura Mashariki, kaunti ndogo ya Fafi, Garissa.

Mkasa huo ulitokea maafisa hao waliposhambuliana kimakosa kila upande ukishuku mwingine kuwa ni wa magaidi.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi eneo la Fafi, George Sangalo alisema kulikuwa na hali ya mkanganyiko kati ya vikosi maalum.

“Lilikuwa kosa. Helikopta iliyokuwa na maafisa kutoka Nairobi ilikuwa inaelekea Bura Mashariki huko Fafi,” akasema Sangalo.

Ni mkasa wa ndugu kupigana na kuumizana kimakosa.

“Konstebo wa polisi alimiminiwa risasi na wanajeshi wawili wa KDF naye akiwashuku kwamba maafisa hao ni wapiganaji wa kundi la kigaidi, naye aliwapiga risasi na kuwajeruhi vibaya,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Afisa huyo wa polisi alikuwa akitembea kwa miguu akitoka katika nyumba moja eneo la mji huo.

Kulingana na ripoti ya polisi, “timu ya maafisa wakuu wakiongozwa na Luteni Jacinta Wesonga na Carey Nyawinda imefika eneo la mkasa huko Bura Mashariki”.

Maganda kadhaa ya risasi zilizotumika yamepatikana na “yatatumika katika uchunguzi zaidi.”

You can share this post!

Huenda asilimia 75 ya kampuni zikafungwa Juni – CBK

Hatima ya Jumwa, Wamalwa yaamuliwa

adminleo