Baada ya mkasa wa Solai, maelfu sasa wanaishi kwa hofu
NA PETER MBURU
Mkasa wa bwawa la Solai ambao uliwaua zaidi ya watu 40 sasa umeamsha hofu ya miaka mingi baina ya maelfu ya wakazi wa kaunti ya Nakuru wanaoishi karibu na mabwawa na ambao wamewahi kushuhudia visa sawia miaka ya mbeleni.
Kwa zaidi ya miaka mitano sasa, wakazi wa maeneo ya Solai, Njoro, Salgaa, Rongai na sehemu za Mau wamekuwa wakilalamika kuwa kampuni za kupanda maua zinawaharibia mashamba, mali na kusababisha vifo vya mifugo kwa kuwachilia maji yenye kemikali kwenye mashamba yao.
Wakazi hao aidha wamekuwa wakilaumu kampuni hizo kwa kuharibu barabara na kusababisha magonjwa na vifo miongoni mwa watoto na watu wazima, kutokana na maji machafu.
Hii, kulingana na wakazi ni licha ya kampuni hizo kuzuia maji ya mito kuwafikia ili kuyaelekeza kwenye mabwawa ya kibinafsi.
Wakazi hao ambao wamekuwa wakitembelewa na Taifa Leo mbeleni walisema usumbufu huo ni mbinu ya wamiliki wa makampuni hayo ya maua ili wakubali kuwauzia mashamba, baada yao kukataa kuondoka.
“Walianza kwa kuwachilia maji machafu kwenye mashamba na kuharibu mimea, kuunda mitaro kwenye mashamba. Tumepoteza mifugo na watoto wetu kuugua hadi tukaamua tumechoka. Tumefanya maandamano lakini bado hatujasaidika,” akasema Bw Bernard Solangai, mkazi wa Solai.
Baadhi ya wakazi wa maeneo mengine kama Rongai wamelazimika kuishi katika hali mbaya zaidi baada ya maji hayo yenye kemikali kuunda mitaro ndani ya nyumba zao na kuzidisha visa vya magonjwa.
Mnamo Februari, kikundi cha wakazi wa Michorui eneo la Njoro walifikisha kampuni moja ya maua kortini kwa uharibifu wa mazingira na mali.
Wakiwakilishwa na wakazi watatu, walifika mbele ya mahakama ya Mashamba na Mazingira, baada ya juhudi zao kusuluhisha mizozo na wamiliki wa kampuni hiyo kukosa kuzaa matunda.
Bi Jane Wagathuitu, Bw Isaac Kamau na Bw Samson Gichuki walidai mbele ya korti kuwa kampuni hiyo, ambayo iko juu yam lima kijijini ilishindwa kujihifadhia maji yake, wala kuyatibu kemikali zake zisiadhiri mashamba yao.
Walisema uchafu iliokuwa ikiwachil;ia kampuni hiyo ulisababisha vifo vya mifugo wao, kuharibu mashamba na barabara na magonjwa.
Karatasi za korti aidha zilionyesha kuwa mnamo 2014, moja ya mabwawa ya eneo hilo liliwahi kuvunja kingo zake na kuua mifugo, kuvunja nyumba na kuharibu mashamba na barabara.
“Washtaki wanaomba kulindwa na korti ili mali yao, mifugo afya na mazingira ya kuishi yaboreweshwe kwa kuzuia uharibifu wa mali,” zikasoma karatasi za korti.
Mnamo Februari, wakazi wa Salgaaa waliandamana kukashifu baadhi ya makampuni kuzuia maji ya mito ili kuyaelekeza kwenye mabwawa yao.
“Tumeondoa vizuizi vyote walivyokuwa wameweka ili kuzuia maji kuwafikia wakazi, haya ni maji ya umma na hatuwezi kukubali kunyimwa haki yetu wakati mifuge yetu inakufa kwa njaa,” akasema Bw Isaiah Lobuni.
Sasa, baada ya mkasa wa Solai, wakazi wa vijiji hivyo wanahofia kuwa huenda wakakumbwa na tukio sawia na kuishia kuangamia.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Jumapili, walisema kuwa wamekuwa wakiishi kwa hofu na sasa imezidishwa na wengi hawana amani.
“Baada ya mkasa wa 2014 ambao ulituulia mifugo na kusababisha uharibifu tele, hatuamini fikra zetu tunapowaza kuwa jambo kama hilo laweza kututendekea,” akasema Bi Jacinta Kimani, mkazi wa Njoro.