Makala

SIHA NA LISHE: Faida za ubuyu

October 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MBUYU ni miongoni mwa miti yenye faida nyingi.

Karibu kila kitu au kila sehemu ya mbuyu ina matumizi na manufaa kwa binadamu ambapo inaweza ikatumika kama chakula au dawa.

Unga wa ubuyu unaelezwa kuwa na vitamini na madini mengi kuliko matunda mengine yoyote yale unayoyajua.

Ubuyu katika mwili una uwezo mkubwa wa kuimarisha kinga ya mwili, kuimarisha mifupa, kusaidia mfumo wa umeng’enyaji chakula tumboni, kupunguza maumivu na uvimbe na kusisimua utengenezaji wa seli na tishu mpya.

Pia husaidia kupunguza shinikizo la damu na kuzuia magonjwa sugu.

Zifuatazo ni faida za unga na juisi ya ubuyu kiafya

Inaelezwa kuwa unga wa ubuyu una Vitamini C nyingi mara sita zaidi ukilinganisha na chungwa.

Ubuyu una kiwango kingi cha madini ya Calcium maradufu ya maziwa ya ng’ombe. Pia madini mengine yapatikanayo katika ubuyu ni pamoja na madini ya Chuma, Magnesium na Potassium ambayo ni mara sita zaidi ya ile Potassium ipatikanayo katika ndizi!

Husaidia kujenga neva za fahamu mwilini.

Huwa na virutubisho vya kulinda mwili.

Ubuyu huwa na madini ya chuma ambapo kimsingi, vyakula vyenye afya zaidi kwa ajili ya mwili wa binadamu huwa pia huwa na Vitamini B2.

Ubuyu huimarisha kinga ya mwili kwa sababu ya kuwa na kiasi kingi cha vitamini C.

Huongeza au kuboresha nuru ya macho.

Husaidia kuzuia kuharisha na kutapika.

Magnesium ndani yake husaidia kujenga na kuimarisha mifupa na meno.

Husaidia wenye presha ya kushuka na wenye matatizo ya figo.

Jipatie kikombe kimoja cha juisi ya ubuyu kila siku hasa usiku na baada ya wiki kadhaa utaona matokeo yake mwilini.

Ili upate faida za juisi ya ubuyu, jinsi inavyoelezwa hapa, lazima upate ule ubuyu halisi usiochanganywa na kitu kingine cha kuongeza ladha au rangi.

Jinsi ya kuandaa juisi yake

Chukuwa unga wa ubuyu, weka kwenye kikombe, ongeza maji na ukoroge vizuri.

Unaweza kuongeza sukari au asali; tikisa na unywe.