Hofu ya ulevi wa jombi yafikisha mke kwa bosi
Na LEAH MAKENA
GIAKI, MERU
MAMA wa hapa alishangaza watu wengi alipozuru ofisi alikokuwa akifanya kazi mume wake ili kupata hakikisho kwamba hakuwa amepigwa kalamu.
Mama alikiri kuwa alishuku mumewe alikuwa amefutwa kazi kwa sababu mara nyingi alionekana kwa mamapima akibugia mvinyo na kila alipomuuliza alidai kuwa alikuwa likizoni.
Habari zasema kuwa mama alisikitishwa na tabia ya mumewe ya kurauka alfajiri kana kwamba alikuwa akienda kazini kisha kukita kambi kwa mamapima mchana kutwa.
Hapo ndipo aliamua kufika kwa bosi kubaini iwapo jamaa alifaa kuwa likizoni baada kukosa kutoa cheti cha kuonyesha alikuwa mapumzikoni.
Siku ya tukio, mama alifika ofisini mapema na kulazimika kusubiri bosi wa mumewe aliyefika mwendo wa saa nne.
Baada ya kukubaliwa kuongea na bosi, mama alifungua roho na kuelezea hofu yake kuhusu tabia ya polo na kukiri kuwa ilimpa wasiwasi ndipo akashuku jamaa alikuwa amepigwa kalamu.
Inasemekana kuwa mama alipata nafuu alipohakikishiwa kuwa jamaa bado alikuwa mfanyikazi wa kampuni hiyo ila bosi akaonya kuwa mwenendo wake ulikuwa unatiliwa shaka na hivyo alitakiwa kurekebisha iwapo hakutaka kumwaga unga.
Hapo ndipo mama alipata nguvu na kuanza mikakati ya kuwafahamisha ndugu za polo wamfanyie kikao ili apunguze ulevi kabla ya kitumbua kuingia mchanga.
Hata hivyo, wosia wa mama ulionekana kama kumpigia mbuzi gitaa kwani polo alikuwa amezama kwenye ulevi na hakuonyesha dalili za kujinasua.
Minong’ono yasema kuwa mama aliapa kufanya vyovyote vile kumtoa kwenye dimbwi la ulevi na akatishia kuondoka iwapo polo asingetambua juhudi zake.