Kwa muda mrefu tumelipwa mishahara ya kitoto, walimu wa chekechea walia
NA WANDERI KAMAU
WALIMU wa shule za chekechea nchini sasa wanataka kuwekwa chini ya usimamizi wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) na kulipwa mishahara kama walimu wengine.
Walimu hao pia wanataka kuwekwa katika viwango mbalimbali vya watumishi wa umma, ili kuwapa nafasi za kuongezwa mishahara na kupandishwa ngazi.
Wakihutubu Alhamisi kwenye Kongamano lao Kuu katika Taasisi ya Kukuza Mitaala Kenya (KICD) jijini Nairobi, walimu mbalimbali walieleza jinsi wengi wao wamekuwa wakiteseka, chini ya usimamizi wa serikali za kaunti.
Walieleza kuwa wengi wao wamekuwa wakipokea mshahara wa chini ya Sh15,000 licha ya baadhi yao kuwa na shahada kutoka kwa vyuo vikuu.
“Tumevumilia kwa muda mrefu, kwani baadhi yetu tunafanya kazi kama vibarua. Hakuna sera wala mwongozo unaosimamia taaluma yetu,” akasema Bw John Lang’at kutoka Kaunti ya Uasin Gishu.
Kulingana na katiba, serikali za kaunti ndizo husimamia elimu hiyo, kwa kuwaajiri walimu na kufadhili shughuli zote zinazohusiana nao.
Na licha ya serikali hizo kupewa mamlaka hayo, hakujakuwa na mwongozo maalum wa usimamizi wake, jambo ambalo walimu wengi wamekuwa wakilalamikia.
Kaunti pia zimekuwa zikifanya maamuzi huru kuhusu viwango vya mishahara ambayo huwa zinawalipa, baadhi zikilaumiwa kwa kuwanyanyasa licha yao kuwa na elimu ya kiwango cha juu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Wilson Sossion, alisema kuwa wanalishinikiza Bunge la Kitaifa kuifanyia mageuzi Sheria Kuhusu Elimu ya Chekechea, ili kubuni mwongozo ambao utahakikisha kuna kanuni sawa zinazosimania mfumo unaotumiwa kuwaajiri.
“Tutashinikiza mageuzi ya sheria hiyo, ili kurahisisha utaratibu wa ulainishaji wa usimamizi na uendeshaji wa elimu hiyo,” akasema Bw Sossion.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Amina Mohammed alisema kuwa serikali imepata ufadhili kutoka kwa Benki ya Dunia, kwa ujenzi wa vituo vine vipya vya utoaji mafunzo kwa walimu wa chekechea.
“Tunalenga kuhakikisha kuwa maslahi ya walimu wa chekechea yameshughulikiwa kwa kuzingatia mwongozo utakaobuniwa baada ya mageuzi ya sheria inayousimamia,” akasema.