Idd-ul-Adha: Usalama waimarishwa Lamu
NA KALUME KAZUNGU
USALAMA umeimarishwa katika kisiwa cha Lamu na maeneo yote ya mpakani mwa Lamu na Somalia wakati huu ambapo waumini wa dini ya kiisalmu wanaadhimisha sherehe ya Idd–ul–Adha kote ulimwenguni.
Naibu Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono (pichani) anasema tayari wamesambaza maafisa wa kutosha wa usalama kila sehemu ambapo waumini wa dini ya kiisalmu wanakongamana kwa sherehe za Idd–ul–Adha.
Akizungumza na Taifa Leo mjini Lamu Jumanne, Bw Rono alisema pia wamehakikisha kila maeneo ambayo yamekuwa yakilengwa na magaidi wa Al-Shabaab, hasa Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na hata sehemu za mpakani, ikiwemo Kiunga na na Ishakani zinalindwa ipasavyo.
Aidha aliwashauri wakazi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha usalama kwenye maeneo yao unadhibitiwa.
“Tayari tumeweka usalama wa kutosha hasa kisiwani Lamu ambapo waumini wa dini ya kiislamu ni wengi. Tutahakikisha doria zinafanywa misikitini, mahotelini, barabarani, baharini na hata angani. Ninawashauri wakazi kupiga ripoti kwa polisi iwapo watashuhudia tukio au mtu yeyote wanayemshuku kuwa kero kwa usalama,” akasema Bw Rono.
Aliwashauri wakazi kuukumbatia mfumo wa Nyumba Kumi katika kukabiliana na wahalifu hasa msimu huu wa Idd–ul–Adha, ambapo k wageni wengi wanatarajiwa kuwasili Lamu kuadhimisha hafla hiyo.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo kisiwani Lamu aidha walisema wamefurahia jinsi usalama ulivyodhibitiwa kote Lamu.
“Idd–ul–Adha ni hafla muhimu kwetu sisi waislamu. Tunawakumbuka wenzetu walioenda kuhiji. Hii ni nguzo muhimu ya imani kwetu waislamu. Pia tunashukuru serikali kwa kudhibiti usalama eneo hili,” akasema Bw Mohamed Bashauf.