Habari za Kitaifa

DCI: Huyu ndiye Gaitho tuliyekusudia kunasa tulipomshika kimakosa mwanahabari Macharia Gaitho


MWANAMITANDAO aliyekuwa akisakwa na polisi waliomtia nguvuni kimakosa mwanahabari wa miaka mingi na mchangiaji makala katika Daily Nation, Macharia Gaitho, ameshtakiwa.

Francis Ng’ang’a Gaitho alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondieki kwa kuchapisha habari za uwongo na za kupotosha kuhusu jina la mshukiwa mkuu katika mauaji ya wanawake eneo la Kware, Embakasi.

Na wakati huo huo, mfanyabiashara Alinur Mohamed Bulle alishtakiwa kujifanya Msemaji wa Ikulu.

Gaitho anayewakilishwa na wakili mwenye tajriba ya juu Dkt John Khaminwa pamoja na mawakili Austin Kitinya na Duddley Ochiel alikana mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya mitandao.

Alikana kwamba mnamo Julai 15, 2024 alichapisha habari katika akaunti yake ya X (Twitter) @FGaitho9237 kwamba idara ya uchunguzi wa jinai lilichapisha jina la mshukiwa mkuu katika mauaji hayo ya Kware kuwa Collins Jumais Khalusia.

Hakimu ilielezwa Gaitho alidokeza kwamba jina la mshukiwa wa mauaji hayo ni Jairus Onkundi, mwanachuo aliyefuzu kutoka chuo kikuu cha kiufundi cha Meru.

Bw Ondieki alifahamishwa zaidi kwamba mshtakiwa alidai katika taarifa aliyochapisha kwamba waeneza uvumi wa serikali walichapisha habari kuhusu mshukiwa huyo na majina yake kabla ya kuyathibitishwa.

Korti ilifahamishwa kwamba lengo la waeneza uvumi wa serikali ilikuwa kupotosha umma ilhali vyombo tanzu vya habari vilikuwa vinakwepa kuchapisha ukweli wa mambo.

Mahakama iliongeza kuelezwa na kiongozi wa mashtaka Everlyne Mutisya kwamba serikali ililenga kupotosha umma kuhusu ukweli wa mauaji ya waandamanaji waliopinga Mswada wa Fedha 2024-2025.

Bi Mutisya alisema mshukiwa huyo amejizatiti kujinasua na kesi hiyo lakini hafui dafu kwa vile ushahidi uliopo umemlenga barabara.

Gaitho, mwenye umri wa 44 alidaiwa alichapisha kwamba ukweli wa maneno utajulikana.

Akiwasilisha ombi la mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana, Dkt Khaminwa alisema mshtakiwa alijisalimisha kwa polisi mnamo Julai 17, 2024.

Alikana mashtaka na kuomba aachiliwe kwa dhamana akisema “niko na mke na watoto na kamwe siwezi kutoroka na kuwaacha.”

Mahakama ilielezwa Gaitho atafika kortini kila atakapohitajika.

Dkt Khaminwa alisema “nitahakikisha kwamba mshtakiwa amefika kortini anapotakiwa.”

Kiongozi wa mashtaka Bi Everlyne Mutisya hakupinga ombi la dhamana akisema “DPP hajaamuru mshtakiwa anyimwe dhamana ambayo ni haki yake kwa mujibu wa Katiba.”

Bw Ondieki alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh30,000.

Aliamuru kesi dhidi ya Gaitho itajwe Agosti 1,2024 kwa maagizo zaidi.

Na wakati huo huo Alinur alikana alisambaza habari katika akaunti yake ya X , @AlinurMohamed mnamo Julai 15, 2024 kwamba “Mimi ni mwanahabari na msemaji wa Ikulu. Siko tayari kuendelea na kueneza uvumi ni heri nipoteze kazi hii #RutoMustGo#, #Anguka nayo#”

Hakimu alielezwa Alinur alijifanya ujumbe huo ulitumwa na msemaji wa Ikuku Hussein Mohamed, MBS, kupitia kitandawazi chake cha “@HusseinMohamedg”

Alinur aliachiliwa kwa dhamana ya Sh30,000.

Kesi itatajwa Agosti 1,2024 kwa maagizo zaidi.