Ni Kenya, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Rwanda kwenye Kundi A la Cecafa U-17 wavulana
KENYA itamenyana na Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Rwanda katika Kundi A kwenye michuano ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la Wavulana walio chini ya miaka 17 (AFCON U-17) ya ukanda wa CECAFA mnamo Novemba 15 hadi Desemba 2 nchini Ethiopia.
Droo ya mashindano hayo ya mataifa 10 ilifanyika Ijumaa, Oktoba 31, 2025 katika studio za FUFA FM mjini Mengo, Uganda, ikiongozwa na Mkuu wa Mauzo na Mawasiliano wa CECAFA, Andrew Oryada.
Oryada alisema kuwa michuano ya Cecafa inawapa wachezaji chipukizi nafasi muhimu ya kuonyesha vipaji vyao katika jukwaa la kimataifa na kujiendeleza kuelekea mashindano ya bara na ya dunia.
Michuano ya Kundi A itachezwa uwanjani Abebe Bikila mjini Addis Ababa. Mechi za Kundi B zinazojumuisha mabingwa watetezi Uganda, Tanzania, Djibouti, Sudan na Burundi, zitaandaliwa uwanjani Dire Dawa.
Timu mbili-bora kutoka kila kundi zitaingia nusu-fainali ambapo washindi watasonga fainali na waliopoteza watapigania medali ya shaba. Bingwa, nambari mbili na tatu watanyakua tiketi kuwakilisha kanda ya CECAFA katika AFCON U-17 mwaka 2026.
Mashindano ya CECAFA ni nafasi nyingine kwa wachezaji chipukizi wa Kenya kushindana katika ngazi ya juu, huku taifa likilenga kurejea kwenye ubora wa soka ya vijana. Kenya haijawahi kushiriki AFCON U-17 tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1995.
Makundi ya CECAFA U-17:
A: Ethiopia, Somalia, Kenya, Sudan Kusini, Rwanda
B: Uganda, Tanzania, Djibouti, Sudan, Burundi
