Hofu Ethiopia ikianza kuuza miraa Somalia
Na DAVID MUCHUI
WAKUZAJI miraa nchini wameeleza wasiwasi kwamba huenda wakapoteza soko la Somalia kabisa, baada ya Ethiopia kuanza kusafirisha zao hilo nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari katika taifa hilo, shirika la ndege la Ethiopia, liliwasilisha shehena ya kwanza ya zao hilo katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Aden Adde, Mogadishu mnamo Jumamosi.
Hali hiyo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakuzaji hao nchini, ikizingatiwa ndio wamekuwa wakidhibiti mauzo ya zao Somalia kwa muda mrefu.
Wakuzaji miraa nchini Ethiopia wamekuwa wakidhibiti soko la Hargeisa. Wakenya walishindwa kupenya soko hilo kutokana na kiwango cha juu cha kodi.
Vyombo hivyo viliripoti kwamba serikali ya Somalia imeiruhusu Ethiopia kuendesha biashara hiyo nchini humo, huku marufuku dhidi ya Kenya ikiendelea kuwepo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakuzaji Miraa cha Nyambene (Nyamita), Bw Kimathi Munjuri, alisema kuwa serikali ya Somalia pia imeimarisha usalama katika Bara Hindi kuhakikisha hakuna miraa kutoka Kenya inaingizwa nchini humo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakuzaji Miraa wa Maua, Bw Mohamed Quresh, alisema serikali ya Somalia pia ilitoa makataa ya siku tatu kwa wafanyabiashara kutoka Kenya ambao wamekuwa wakiingiza zao nchini humo kupitia Mandera kukoma kufanya hivyo mara moja.
Bw Munjuri aliiomba serikali ya Kenya kufanya mazungumzo na Somalia ili kuwarejeshea udhibiti wa soko hilo.
“Hapo awali, miraa ya Ethiopia haikuwa ikisafirishwa Somalia. Ikiwa watumizi wake wataruhusiwa kuzoea miraa kutoka Ethiopia, huenda tukapoteza soko hilo kabisa. Zaidi ya mashua 50 zimetumwa eneo la mpakani Bara Hindi kutuzuiwa kuingia humo. Mbona serikali yetu imeruhusu Ethiopia kuingilia soko letu?” akashangaa.
Akaongeza: “Tunafahamu kuwa Jumapili, zaidi ya tani 30 za miraa ziliwasilishwa Mogadishu.”
Alisema wakulima sasa wamechoshwa na mkwamo huo ambao umedumu kwa miezi saba. Alisema wengi wao wanakumbwa na matatizo ya kifedha.
Kwa mujibu wa Bw Quresh, mashirika ya ndege ambayo yalikuwa yakisafirisha zao hilo Somalia sasa yanatathmini kuhamia nchini Ethiopia, ambako kiwango cha biashara kinatarajiwa kuwa cha juu.
Alisema kuna masharti makali ambayo yametolewa na Somalia, miraa yoyote kutoka Kenya iliyo katika taifa hilo kuondolewa.
“Tumefahamu kwamba miraa kutoka Ethiopia inauzwa kwa bei rahisi huku inayobaki ikirejeshwa kwa wakulima. Wafanyabiashara wengi sasa wanatathmini uwezekano wa kuhamia Somalia. Mpango huo unalenga kutuondoa kabisa nchini humo. Hali ilivyo kwa sasa, ni Rais Uhuru Kenyatta pekee anayeweza kuokoa sekta hii,” akasema.
Bw Quresh alisema hali hiyo imeathiriwa zaidi na uchaguzi wa urais unaokaribia nchini humo.