Habari Mseto

Ajiua kwa kunyimwa hela za mvinyo na mkewe

June 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

KIJANA wa miaka 39 katika kaunti ya Murang’a amejitoa uhai baada ya kupandwa na hasira ya kunyimwa pesa za kununua pombe na mkewe.

James Kamau kutoka kijiji cha Mbogo-ini kilichoko katika wadi ya Kahumbu aliafikia uamuzi huo usiku wa kuamkia Jumatano.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua mwanamume huyo alikuwa ameshida katika mtaa wa Mbogo-ini akitoa miche za parachichi ambazo serikali ya kaunti hiyo inapea wakulima.

‘Kuna mradi wa gavana Mwangi wa Iria ambao unalenga kutoa miche milioni moja kwa wakulima 250, 000 wa kaunti hiyo. Bw Kamau ambaye tunaongea kuhusu kujiua kwake ndiye alikuwa akishirikisha utoaji wa miche hiyo katika mtaa huo,” akaambia Taifa Leo Dijitali.

Aliongeza kuwa Bw kamau hata yeye alijipa miche kadhaa na ambayo alichukua kibarua mmoja na wakaandamana naye hadi shambani lake na wakaipanda.

“Ndipo Bw kamau aliamua kuburudika katika baa moja ambayo iko karibu na nyumbani kwake. Aliandamana na yule kibarua wake…Walinunua lita mbili za pombe aina ya Senator Keg na Kamau ndiye aligharamia,” asema.

Kamanda huyo aliongeza kuwa duru za mashahidi ziliarifu kuwa “ni kama Bw Kamau hakutosheka na pombe hiyo na akawa amemaliza pesa alizokuwa amebeba.”

Ndipo, yaripotiwa, alitoka na akarejea nyumbani mwendo wa saa nne usiku na akamuomba bibi yake pesa.

“Bw kamau amekuwa mfanya biashara ambaye katika siku za hivi karibuni haikuwa ikiwmendea vyema. Naye bibi yake huwa na duka la kuuza bidhaa…Inasemwa kuwa bibi alikataa kutoa pesa za kufadhili ulevi,” akasema Bw Kinyua.

Ndipo kwa hasira Bw Kamau alizua fujo akitaka apewe pesa kwa lazima. “Tumepata taarifa kuwa baada ya mamake Kamau kusikia vurugu hilo, alikimbia na akadadisi hali akaona fujo hizo zilikuwa na ukali mwingi…Mamake Kamau alimchukua bibi huyo na akampa malazi..Kwa hasira, Kamau alisikika akionya mamake kuwa alikuwa na mapendeleo kwa bibi huyo na akaapa kuwaadhibu wote wawili kwa maombolezi,” asema kamanda huyo.

Inaarifiwa kuwa Bw Kamau alirejea kwa nyumba yao ambapo watoto wao watatu walikuwa usingizini, akafunga mlango na asubuhi yake watoto walipoamka, wakamwona baba yao akining’inia kutoka kwa paa la nyumba sebuleni.

Walifungua mlano na kutoa habari hizo na ndipo ilibainika kuwa Bw Kamau tayari alikuwa marehemu na ambaye alipelekwa hadi Mochari ya Murang’a kuhifadhiwa.

Hayo yakawa masaibu ya kusombwa na mawazo, kujaribu kuyatuliza kwa ulevi na kufeli, kijisababu cha kunyimwa pesa ba mkewe kikatumika kama basi la kujisafirisha hadi kuzimu—janga la kijamii.