Mwalimu mkuu aanguka na kufa ghafla akiwa afisini mwake
Na MWANGI MUIRURI
WINGU la simanzi limetanda katika shule ya upili ya Mukuria iliyoko eneo bunge la Kandara, Kaunti ya Murang’a baada ya mwalimu mkuu kuanguka ghafla na kuaga dunia akiwa afisini mwake.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ndogo ya Kandara Bw Peter Maina, mwalimu huyo akitambuliwa kama Bi Faith Mureithi alikuwa amefika katika shule hiyo asubuhi akiwa mzima wa afya.
“Lakini habari tulizo nazo ni kwamba mwalimu huyo alianza kuhisi unyonge na ndipo akaingia afisini mwake kutulia,” akasema Bw Maina.
Aliongeza kwamba “muda mfupi baadaye walimu wengine walisikia kishindo katika afisi ya mwalimu wao mkuu na walipoingia kujua kiini, wakakumbana naye akiwa hoi sakafuni”.
Bw Maina alisema kwamba harakati za kumpa huduma ya kwanza ziliingiwa na taharuki baada ya kugundua hakuwa akipumua.
“Alikimbizwa katika hospitali iliyo karibu na baada ya kutambulika alikuwa ameaga, mwili wake ukapelekwa hadi mochari ya Montezuma Monalisa iliyoko katika mtaa wa Kabati,” akasema.
Bw Maina alisema kwamba kisa hicho kinashughulikiwa kama mauti ya ghafla.
“Hata hivyo, tumetuma maafisa wetu wa uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) ili kutekeleza uchunguzi wa kina na hatimaye tupewe ripoti ya uhakika kuhusu mauti hayo ya kusikitisha,” akasema.
Alisema kwamba ripoti ya upasuaji wa mwili ili kubaini kiini hasa cha mauti ndiyo itatoa taswira kamili.
Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika bunge hilo alisema kwamba amewasiliana na wadau katika shule hiyo na kuwasilisha risala zake za rambirambi.
Bw Nyutu alisema kwamba kwa sasa juhudi za kuandaa mikutano ya wadau zimeanza ili mwalimu huyo apewe heshima zake za mwisho.
Waziri wa Ardhi Bi Alice Wahome ambaye alihudumu kama mbunge wa Kandara kati ya 2013 na 2022 alitoa risala zake za rambirambi akimtaja mwendazake kama “mzalendo, mpole na mwenye kujituma kuhudumia sekta ya elimu eneo hilo”.