Mwanamke azuiliwa kwa kuua na kutupa mtoto wa wiki mbili katika shamba la mahindi
MWANAMKE mwenye umri wa 28 anazuiliwa na polisi katika eneo la Rachuonyo Kaskazini kwa madai ya kumuua mtoto wake wa wiki mbili kabla ya kuutupa mwili wake kwenye shamba la mahindi.
Mshukiwa alikamatwa karibu na kituo cha biashara cha Kadel baada ya kukabiliwa na majirani zake.
Mwanamke huyo, mama wa watoto wanne, baadaye anadaiwa alikiri kumuua mtoto wake.
Hapo awali alionekana akiwa amembeba mtoto ndani ya eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Kaskazini, Lydia Parteyie alisema hakuna mtu aliyeshuku kuwa angemuua mtoto wake mchanga.
‘Mashahidi walisema alionekana akienda kwenye shamba la mahindi akimbeba mtoto mgongoni,’ alisema.
Baadaye mshukiwa alionekana akitoka kwenye shamba hilo lakini alikuwa akitembea peke yake bila mtoto.
“Waliomuona walimshuku na kuamua kumuuliza alipo mtoto wake, alisitasita na hakutaka kuzungumza lolote wakati wananchi walipotaka kujua mtoto huyo yuko wapi,” alisema.
Baadhi ya wakazi waliamua kumvamia ili aweze kufichua alipo mtoto wake.
Bi Parteyie alisema alipata majeraha wakati wa shambulio hilo.
Hatimaye alikiri kuwa alimuua mtoto huyo na kutoa taarifa za jinsi alivyotekeleza mauaji hayo.
Wakazi pia walimtaka awapeleke ulipokuwa mwili wa mtoto mchanga na mshukiwa alikubali kuwaongoza hadi eneo la uhalifu.
Mshukiwa huyo baadaye alipelekwa katika kambi ya Polisi ya Kadel ambapo alizuiliwa kwa muda kabla ya kuhamishwa hadi Kituo cha Polisi cha Kendu Bay.
IMETAFSIRIWA NA SAMMY KIMATU