Habari Mseto

Rais awavulia kofia wenyeji eneo la Solai

May 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

WAKAZI wa Solai, Kaunti ya Nakuru wamesifiwa kuwa mashujaa kwa ujasiri walioonyesha walipookoa wenzao wakati bwawa lilipopasua kuta zake na kusababisha vifo vya watu 47 wiki iliyopita.

Viongozi mbalimbali waliozungumza wakati wa ibada iliyofanywa katika uwanja wa Kanisa la AIC Solai Jumatano wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, walisema ujasiri wa wakazi ulisaidia kuokoa maisha ya wengi usiku wa Jumatano iliyopita.

“Nashukuru wakazi wa Solai vile mlijitokeza kwa hali na mali kusaidia wenzenu usiku wa manane. Shida ilipotokea hamkusita wala kusema “mimi niko sawa”. Mlijitokeza na kuona jinsi kila mtu angesaidia mwenzake. Huo ni moyo wa Ukenya,” akasema rais.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo wabunge, maseneta, magavana, madiwani na mawaziri.

Gavana wa Nakuru, Bw Lee Kinyanjui, alieleza jinsi wakazi walivyovumilia hali ngumu usiku huo kuokoa wenzao hadi wanajeshi wa taifa (KDF), maafisa wa shirika la Kenya Red Cross na wataalamu wengine wa uokoaji walipowasili.

Kulingana na Bw Kinyanjui, minara ya kusambaza umeme iliangushwa na maji hivyo kukawa na giza, na barabara hazingepitika kwa magari kwani zilijaa maji.

“Jamii ya Solai ilifanya mambo ambayo hakuna mtu angedhani wangeweza. Walienda zaidi ya kilomita moja ndani ya maji kuokoa waathiriwa gizani bila usaidizi wa kitaalamu. Ingawa tunaomboleza walioaga, wale ambao waliokolewa ni wengi na tunashukuru,” akasema Bw Kinyanjui.

Hata hivyo, alisema sasa kuna jukumu kubwa la kuanza kujenga upya eneo hilo kwani mbali na uharibifu wa mijengo yote, ardhi iliharibiwa kwa kiasi ambacho itakuwa vigumu kuendeleza kilimo.

Alifichua magavana wote wamekubaliana kila kaunti ipeane Sh100,000 kwa hazina ya kusaidia wakazi wa Solai. Hiyo ni Sh4.7 milioni kwa jumla.

Mbunge wa Subukia ambako Solai inapatikana, Bw Samuel Kinuthia, alitoa wito kwa wahisani wazidi kusaidia waathiriwa.

Kwa upande wake, Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika, alisema kuna familia zaidi ya 500 zitakazohitaji makao mapya kwa dharura.

Naibu wa Rais alitaka kila mwananchi ajitwike jukumu la kutunza mazingira kama njia moja ya kuzuia majanga kama vile mafuriko ambayo yamesababisha maafa mengi kitaifa.

“Najua wakati kama huu tunaweza kuanza kujiuliza ni kwa sababu gani haya yalifanyika, nani alikuwa na makosa lakini nataka tujiulize kama Wakenya ni nini kila mmoja wetu angefanya kibinafsi ili tuzuie majanga kama haya yasifanyike tena katika taifa letu,” akasema Bw Ruto.

Serikali iliahidi itasaidia wananchi katika pembe zote kitaifa ambao wameathirika na mafuriko katika msimu huu wa mvua.