Wailaumu serikali ya kaunti kukosa kuwanasua kutokana na minyororo ya mihadarati
NA KALUME KAZUNGU
WAATHIRIWA wa ulanguzi wa dawa za kulevya eneo la Lamu wanailaumu serikali ya kaunti hiyo kwa kuwatelekeza katika kuwasaidia kujinasua kutoka kwa janga hilo.
Waathiriwa hao wanadai serikali ya kaunti haijatoa mbinu zozote mwafaka za kuwasaidia kujinasua kutoka kwa maisha ya uteja licha ya waathiriwa hao kuwa tayari kubadili tabia.
Wakizungumza na wanahabari mjini Lamu Alhamisi, mateja hao walisema baadhi ya maafisa wa kaunti wamekuwa wakiwatafuta na kusajili majina yao kwa lengo la kuwasaidia na kisha kutoweka baadaye.
Wakiongozwa na Bi Khadija Shebwana, mateja hao walieleza hofu yao kwamba wanaowaandikisha majina huenda wanafsnya hivyo ili kujinufaisha wenyewe binafsi.
Walimuomba Gavana wa Lamu, Fahim Twaha, kuandaa mkutano wa dharura na mateja hao ili kuwapa fursa ya kumweleza masaibu yao na kutafuta jinsi atakavyowasaidia.
“Mimi nimekuwa teja kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita baada ya wazazi wangu kutalakiana, hivyo kukosa malezi bora. Niko tayari kuachana na dawa za kulevya iwapo wahisani watajitokeza kutusaidia. Kaunti imetutelekeza.
Majina yetu yamekuwa yakichukuliwa mara kwa mara na kuahidiwa kwamba tungesaidiwa lakini hakuna lolote limefanywa kufikia sasa. Ningemuomba gavana wetu, Fahim Twaha, kutufikiria sisi mateja kwani pia ni binadamu kama wengine,” akasema Bi Khadija.
Naye Bw Ali Islam aliitaka kaunti kubuni vituo vya urekebishaji tabia kwa walanguzi wa dawa za kulevya.
Alisema wengi wao wako tayari kuacha kutumia mihadarati iwapo vituo kama hivyo vitabuniwa kuwasaidia kubadili tabia.
“Tunaambiwa kaunti iko mbioni kuanzisha kituo cha urekebishaji tabia kwa walanguzi wa dawa za kulevya eneo la Hindi. Hakuna yeyote ambaye amejitokeza kutueleza maendeleo ya mpango huo. Ombi langu ni kwamba serikali iharakishe ujenzi wa vituo vya urekebishaji tabia kwa walanguzi wa dawa za kulevya hapa Lamu,” akasema Bw Islam.
Akizungumza na Taifa Leo aidha, Naibu Gavana wa Lamu ambaye pia ni Waziri wa Idara ya Elimu, Masuala ya Vijana na Michezo, Abdulhakim Aboud, alipinga madai ya kaunti kuwatelekeza waathiriwa wa mihadarati.
Badala yake, Bw Aboud alisema kupitia usaidizi wa Shirika la Kimataifa kuhusiana na Masuala ya Mihadarati (UNODC), tayari wameanzisha mpango unaolenga kuwasaidia waathiriwa wa mihadarati kuacha uraibu huo kote Lamu.
“Ni kweli. Tumesajili majina ya waraibu wa mihadarati hapa Lamu. Kwa ushirikiano na UNODC, tuko mbioni kubuni kituo cha kuwasaidia waathiriwa wa mihadarati kuacha uraibu.
Kituo hicho kitakuwa karibu na hospitali ya King Fahad mjini Lamu na tuko asilimia 50 kukamilisha mpango huo. Tayari maafisa watakaoshughulikia mateja hao wamepokezwa mafunzo na hivi karibuni tutafungua rasmi kituo hicho,” akasema Bw Aboud.
Naye Waziri wa Afya wa Kaunti ya Lamu, Raphael Munyua, alisema pia wamekuwa wakiendeleza mpango wa kuwapa tiba maalum wathiriwa wa mihadarati wanaogonjeka ili kuwasaidia kuacha kiu yao ya dawa za kulevya.
“Mpango unaoendelea katika hospitali kuu ya King Fahad unalenga hasa mateja wagonjwa. Tunawaleta hospitalini na kuwadunga sindano ya methadone ambayo huwasaidia kupoteza hamu ya mihadarati,” akasema Bw Munyua.