Habari MsetoSiasa

Ziara za Ruto si tisho kwa ODM – Raila

June 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Raila Odinga, amesema hatishwi na jinsi Naibu Rais William Ruto anavyoonekana kupenya katika ngome zake za kisiasa.

Bw Odinga Jumatano alisema ODM imeweka kipaumbele juhudi za kuleta marekebisho ya mbinu za uongozi kwa manufaa ya wananchi kufuatia muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Alikuwa akijibu ripoti kwamba chama hicho kimeandaa mkutano wa wabunge wake na Kamati Kuu ya Kitaifa ili kupanga mikakati ya kukabiliana na juhudi hizo za Bw Ruto.

“Mkutano uliopangwa hautokani na uoga wala matukio yoyote ya kisiasa yanayoendelea. ODM haifanyi kampeni za 2022 wala haitishwi na wale ambao wameanza kampeni,” akasema kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake Bw Dennis Onyango.

Kwa miezi kadhaa sasa, Bw Ruto amekuwa akiendeleza msururu wa ziara maeneo tofauti nchini hasa Pwani na Magharibi ambapo idadi kubwa ya wapigakura ni wafuasi wa Bw Odinga, kwa msingi wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka uliopita.

Hata hivyo, wakati Rais Kenyatta alipogusia ziara hizo wiki chache zilizopita na kusema Bw Ruto “anatangatanga vichochoroni”, naibu rais alijibu kwa kusema huwa anaenda mashinani kupeleka maendeleo.

Kufikia sasa, baadhi ya wanachama wa ODM waliokuwa mstari wa mbele kukashifu serikali ya Jubilee kabla ya uchaguzi wa mwaka uliopita hasa katika maeneo ya Pwani, wamegeuka na kusema watamuunga mkono Bw Ruto kuwania urais mwaka wa 2022.

Bw Odinga alitofautiana na msimamo wa Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna kwamba wanachama wanaompigia debe Bw Ruto wataadhibiwa, akisema hakuna vile wanachama wanaweza kuadhibiwa ilhali kipindi cha kampeni hakijatangazwa rasmi.

Viongozi wa ODM Pwani walimpuuzilia mbali Bw Sifuna na kusema wanapotangaza kuungana na Bw Ruto wanafuata nyayo za Bw Odinga ambaye aliungana na Rais Kenyatta.

“Chama hakitanyamazisha wanachama wake katika mienendo yao. Hata hivyo, wakati kipindi cha kampeni kitakapofika kisheria, ODM itaamrisha wanachama wake wote waunge mkono mgombeaji wake,” akasema.

Wakati chama hicho kilipofanya mkutano wake wa NEC mara ya mwisho Mei 8, Bw Odinga alisema shughuli zao kwa sasa hazitahusu siasa za 2022 kwani muafaka kati yake na Rais Kenyatta haukukusudia kupanga mikakati ya 2022.

Hata hivyo, muafaka huo uliibua mihemuko mpya wa kisiasa na kufanya vigogo wa kisiasa wa maeneo mbalimbali kitaifa waanze kujiandaa kwa uchaguzi ujao wa urais.

Bw Sifuna jana alieleza kuwa onyo alilotoa kwa wanachama wanaompigia debe Bw Ruto lilinuiwa kuwakumbusha msimamo wa chama kuhusu kusitisha siasa za 2022 kama walivyoshauriwa na Bw Odinga awali.

“Ninachowaambia ni kuwa unaweza kudhani unampuuza Sifuna lakini ukweli ni kwamba unakosea heshima chama chako,” akasema.

Aliongeza kuwa mkutano wa chama utakaofanywa wiki ijayo utalenga kuwasisitizia wanachama kuhusu malengo muhimu zaidi ya chama kwa sasa ili wasonge mbele kwa pamoja.

Kulingana na Bw Sifuna, ODM haina sababu ya kuhofia chochote kwani hata kabla ya uchaguzi wa 2017 kulikuwa na wanachama wakaidi Pwani ambao baadaye walishindwa uchaguzini walipojiunga na serikali.