Kibarua kizito cha upinzani 2027 ikiwadia
MAZUNGUMZO ya vinara wa upinzani yanaashiria kibarua kizito cha kuunda muungano imara utakaomkabili Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027.
Huku uchaguzi ukisalia takriban miezi 10, viongozi hao wanakabiliwa na changamoto ya kukubaliana kuhusu mgombea mmoja wa urais, mgombea mwenza, uwiano wa kikanda na namna ya kuwavutia vijana wa Gen Z.
Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, alisema Jumatatu baada ya kukutana na kiongozi wa DCP, Rigathi Gachagua, nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri, kwamba upinzani hautakata tamaa katika juhudi za kuungana.
“Tuna dhamira ya kuendelea kutafuta umoja,” alisema Kalonzo.
Gachagua naye alisema njia ya uhakika ya kumshinda Dkt Ruto ni kuafikiana kuhusu mgombea mmoja wa urais.
“Tumekubaliana kuwa kumpata mgombea mmoja wa urais ndiyo njia ya uhakika ya kushinda uchaguzi mkuu ujao. Sote tumejitolea kufikia lengo hilo,” alisema Gachagua.
Aliongeza kuwa viongozi wako tayari kujitolea ili kumpata mtu atakayeongoza juhudi zao za kisiasa.
Hata hivyo, kukubaliana kuhusu mgombea huyo kunatarajiwa kuwa kazi ngumu kwa sababu viongozi wengi wana malengo ya kuwania urais. Pia wanahitaji kumpata mtu anayeweza kuvutia wapigakura katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Utafiti wa Trends and Insights for Africa (Tifa) wa Julai ulionyesha kuwa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alikuwa na uungwaji mkono wa asilimia 15 iwapo angewania urais. Rais Ruto alikuwa na asilimia 24, huku aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i akiwa na asilimia 14 na Kalonzo asilimia 13. Gachagua alikuwa na asilimia saba.
Viongozi pia wanapaswa kuzingatia uwezo wa kifedha, mitandao ya kisiasa na miundo ya kampeni ya kila mgombea.
Eneo la Mlima Kenya ni muhimu kutokana na idadi yake kubwa ya wapigakura na mchango wake katika ushindi wa Ruto mwaka 2022. Kwa hivyo, nafasi ya mgombea mwenza inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mazungumzo ya upinzani.
Tikiti ya Kalonzo na Sifuna imetajwa katika tafiti za hivi karibuni kuwa miongoni mwa zinazovutia. Hata hivyo, viongozi bado wanahitaji kuafikiana kuhusu namna ya kusawazisha maslahi ya maeneo mbalimbali.
Seneta wa Kitui Enoch Wambua anasema mgombea wa pamoja anapaswa kutangazwa mapema ili awe na muda wa kutafuta rasilimali na kujenga miundo ya kisiasa.
“Wakenya wanahitaji kujua mapema atakayemkabili Ruto kwenye kura. Nasikia kuna makubaliano ya karibu kwamba upinzani utawapa Wakenya zawadi ya Krismasi kwa kutangaza mgombeaji kabla ya mwisho wa mwaka,” alisema.
Naibu kiongozi wa Jubilee, Jeremiah Kioni, alisema baadhi ya viongozi wana uwezo wa kuvutia wapigakura lakini huenda wasiaminike kuongoza nchi, huku wengine wakiwa na sifa za uongozi lakini wakikosa nguvu za kuvutia kura.
Vijana wa Gen Z pia ni sehemu muhimu ya hesabu za upinzani. Wachambuzi wanasema baadhi yao wanaweza kutaka mwelekeo mpya badala ya viongozi ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu.
Katika eneo la Magharibi, Sifuna na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa wanaonekana kushindania ushawishi. Wamalwa alitembelea Gachagua Jumatatu akiwa na wazee, siku chache baada ya Sifuna kufanya ziara kama hiyo akiwa na wafuasi wa vuguvugu la Linda Mwananchi.
Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, aliyekuwa mbunge wa Tongaren Eseli Simiyu na Wafula Wamunyinyi ni miongoni mwa viongozi wa eneo hilo waliounga mkono Sifuna.
Mlima Kenya nako, DCP inashindana na Jubilee ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, PPK ya Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na PLP ya Martha Karua.
Kaimu Katibu Mkuu wa DCP, John Methu, alisema chama kitachunguza vyama vinavyotaka kujiunga na upinzani ili kuhakikisha havitumiki kusababisha migawanyiko.
Kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi alisema licha ya changamoto za kujenga muungano, lengo kuu ni kumuondoa Ruto madarakani kupitia kura na kurejesha utawala bora na kuheshimu Katiba.
Rasimu ya mfumo wa kushirikiana inaonyesha kuwa muungano unapanga kuwasilisha makubaliano yake kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kufikia Machi 31, 2027. Makubaliano ya kugawana nyadhifa yanatarajiwa kukamilishwa kufikia wiki ya mwisho ya Machi.
Rasimu hiyo pia inapendekeza vyama kugawana maeneo ya kuwania viti, ili kila chama kiweke wagombea katika maeneo ambako kina ushawishi mkubwa. Ramani ya mwisho ya maeneo hayo inapangwa kukamilishwa mwishoni mwa Februari 2027.
Hata hivyo, Gachagua amepinga hadharani mpango huo wa kugawana maeneo, akisema ni kiti cha urais pekee kinachopaswa kutokuwa na ushindani wa ndani ya muungano.
Mpango huo umekuwa ukizua utata katika miungano ya awali. Mwaka 2022, Raila Odinga alilazimika kuachana nao baada ya vyama vidogo kutishia kujiondoa katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.
Kiongozi wa DAP-K Wamalwa alisema kujenga muungano si tukio la mara moja bali ni mchakato wa mashauriano na mazungumzo endelevu, akitoa mfano wa muungano wa NARC uliomsaidia Mwai Kibaki kushinda uchaguzi wa 2002.
Kwa sasa, changamoto kuu kwa upinzani ni kubadilisha matamshi ya umoja kuwa makubaliano kuhusu mgombea, nafasi za uongozi na kugawana maeneo kabla ya muda wa uchaguzi kuwadia.