Habari za Kitaifa

Licha ya kuupinga, Ruto amezindua mpango unaofanana na Kazi Mtaani ya Uhuru

Na NDUBI MOTURI September 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amezindua mpango wa kushughulikia hali ya anga unaofanana na mpango wa Kazi Mtaani wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Ameanza mpango huu kuwa mbinu ya kuunda nafasi za kazi kwa mamilioni ya vijana ambao hawajaajiriwa nchini.

Katika mpango huo uliojiri kabla ya maadhimisho ya siku ya kupanda miti, rais alisema vijana watahusishwa katika kusafisha mito iliyochafuliwa, kupanda miti na kuboresha sehemu za kubarizi mijini.

Awamu ya kwanza ya mradi huo kwa jina Climate WorX Initiative itaanza Oktoba 1 katika jiji kuu la Nairobi na italenga vijana 20,000 watakaowekwa kwenye vituo kando ya Mto Nairobi.

Watatwikwa jukumu la kufufua mto huo kwa kupanda miti ukingoni mwake na kutengeneza maeneo ya kubarizi jijini.

“Ninatoa wito kwa machifu wetu wafanye kazi nasi na kuhakikisha tunawapa kipaumbele watu wanaoishi karibu na hapa. Mabadiliko ya hali ya anga ni tatizo kuu lakini kama nchi, ni sharti tujifunze jinsi ya kutumia nafasi zinazotokana na changamoto hii,” alisema Kiongozi wa Nchi katika uzinduzi huo Korogocho.

Majiji yote

Awamu ya pili ya mradi huo itazinduliwa baadaye katika majiji makuu kote nchini — ikiwemo Kisumu, Mombasa, Nakuru na Eldoret.

Vijana watahitajika kutoa suluhisho kwa matatizo yanayohusu mabadiliko ya hali ya anga yanayokabili nchi.

Uzinduzi wa mradi huo umejiri mwaka mmoja baada ya uzinduzi wa Tume ya Mito ya Nairobi na miezi michache baada ya serikali kubomoa nyumba zilizokuwa zimejengwa katika maeneo ya chemchemi ya maji.

Dkt Ruto alisema familia zilizofurushwa kutoka kingo za mto zitapatiwa kipaumbele katika mpango wa nyumba za bei nafuu zinazoelekea kukamilishwa katika muda wa miezi michache ijayo.

Rais alionya viwanda vilivyo kando na kingo za mto kuhusu uchafuzi wa mazingira.

“Tunahitaji kuwa makini kudhibiti mabadiliko ya hali ya anga. Viwanda vinavyochafua mito yetu vitawajibikia. Ni sharti vilipie gharama ya kumwaga uchafu katika mito yetu,” alisema.

Mradi wa Dkt Ruto kuhusu mabadiliko ya hali ya anga unafanana na mpango wa Kazi Mtaani wa Bw Kenyatta ambao Dkt Ruto aliukosoa na kuutupilia mbali alipoingia ikulu.

Kwa jumla, mpango huu unalenga kuajiri angalau Wakenya laki mbili kote nchini.