Habari za Kitaifa

Madiwani wa Gusii wasuta kimya cha Matiang’i kuhusu urais 2027

Na KEVIN CHERUIYOT March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya Madiwani kutoka jamii ya Abagusii kutoka kaunti tatu za Kisii, Nyamira na Nairobi wamemtaka aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i akome kushika mateka jamii hiyo na atangaze iwapo atawania urais mnamo 2027.

Madiwani hao wamemtaka Dkt Matiang’i akome kumtumia Seneta wa Kisii Richard Onyonka kupitisha ujumbe wake kisiasa wakisema seneta huyo ni broka anayesaka maslahi yake ya kibinafsi.

Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi Moses Ogeto Jumatano alimtaka Dkt Matiang’i ajitokeze na kutangaza kama atawania urais badala ya kufanya jamii iamini hivyo ilhali hajatoa tangazo hilo mwenyewe.

Bw Ogeto aliwaongoza madiwani kutoka kaunti hizo kukutana na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga na kumwomba msamaha kutokana na kisa cha Jumapili ambapo alizomewa uwanja wa Gusii.

“Hatukuzungumza kuhusu Dkt Matiang’i katika mkutano wetu. Tutazungumza aje kuhusu mtu ambaye hajatangaza atawania urais?” akauliza Bw Ogeto.

“Kama Matiang’i anataka kuwania urais, basi ajitokeze na azungumze kama kiongozi badala ya kutuma wanasiasa mabroka kama Seneta Onyonka,” akasema Bw Ogeto.

Jumapili Bw Odinga alikuwa amehudhuria hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za Shabana alipopigiwa kelele na vijana waliomsifu Dkt Matiang’i na kupinga muafaka kati ya Raila na Dkt Ruto.

Bw Ogeto aliitaka jamii ya Gusii kufuata mwelekeo wa kiongozi mwenye hadhi ya kitaifa kama Raila ili kunufaikia miradi ya serikali badala viongozi ambao hawajatangaza msimamo na hawajui mwelekeo wao kisiasa.

“Kilichotokea Jumapili ni kisa kilichopangwa na hakina nia njema kwa jamii ya Abagusii. Raila ni kiongozi wetu, tumekuwa nyuma yake na hajalitoroka kabila letu,” akaongeza Bw Ogeto.

Kiongozi wa wengi kwenye Bunge la Kaunti ya Nyamira George Abuga alisema jamii ya Abagusii inamheshimu Raila ndiposa ODM imekuwa ikitawala siasa za eneo hilo kwa kipindi kirefu.

Naye seneta wa zamani wa Nyamira Walter Mong’are alisema tukio hilo halikufaa kwa kuwa jamii ya Abagusii pia inaishi maeneo mengine ya nchi na inaweza kulipiziwa kisasi kutokana na tukio hilo.

“Mtu ambaye wanamzungumzia hatujamwona wala kumsikia akisema atawania urais. Hata kama atakuwa debeni hawezi kushinda kupitia kura zetu pekee,” akasema Bw Mong’are.

Mnamo Machi 6 akiwa Kaunti ya Kisii, Bw Odinga alionekana kutounga mkono uwanizi wa Dkt Matiang’i akisema kuwa hawezi kuchaguliwa kwa kura za eneo la Gusii pekee yake.

“Matiang’i hadi sasa hajasema iwapo atawania urais na hakuna jambo kama jamii inatoa mwaniaji kwa sababu yeyote anagombea anasaka kuongoza Kenya.

“Huwezi kuchaguliwa kama rais kutokana na kura za Abagusii, Waluo, Waluhya na hata Mlima Kenya,”  akasema Bw Odinga.

Uwanizi wa Dkt Matiang’i japo umeidhinishwa na Jubilee, bado umegawanya upinzani Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wakionekana kutomchangamkia.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo