Habari za Kitaifa

Mipango yaendelea kubadilisha kikosi cha Kenya kilichoko Haiti na kingine

Na  NYABOGA KIAGE August 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Kuna mipango ya kuondoa kikosi kinachoongoza na Kenya  kurejesha amani nchini Haiti, na kukibadilisha na kikosi kipya kitakachoitwa Gang Suppression Force (GSF), ambacho kitakuwa na jukumu mahsusi la kupambana na magenge ya wahalifu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wiki hii, Amerika na Panama zimewasilisha pendekezo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) na Shirika la Mataifa ya Amerika (OAS) kuunda kikosi hicho kipya kitakachojumuisha maafisa wa usalama kutoka mataifa mbalimbali.

Inaripotiwa kuwa muda wa kikosi kinachoongozwa na Kenya unakamilika wiki ya kwanza ya Oktoba, na hivyo kuna nia ya kubadili muundo na mbinu za operesheni hiyo.

Hata hivyo, haijabainika wazi tofauti kati ya majukumu ya GSF na yale ya kikosi cha sasa, kwani vyote vinapangiwa kukabiliana na magenge ya uhalifu nchini humo.

Amerika na Panama zimetangaza kuwa zinaandaa mpango rasmi utakaofafanua majukumu, muundo na mbinu za GSF.

Kwa mujibu wa pendekezo hilo, GSF itakuwa na maafisa zaidi ya 5,500 na italenga kumaliza kabisa magenge yanayohangaisha taifa hilo, hasa kundi la Viv Ansanm linaloongozwa na Jimmy Cherizier maarufu kama Barbecue.

Kaimu Balozi wa Amerika katika Umoja wa Mataifa, Bi Dorothy Shea, alisema Kenya imekuwa mshirika muhimu katika operesheni hiyo tangu ilipoanza Juni 2024.

“Tunashukuru Kenya kwa kujitokeza wakati muhimu na kuongoza kikosi cha mataifa mbalimbali kwa zaidi ya mwaka mmoja. Bila juhudi hizo, magenge ya wahalifu yangekuwa yameimarika zaidi,” alisema Bi Shea.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametaka Baraza la Usalama kuidhinisha kikosi cha kimataifa kitakachosaidia kuleta utulivu Haiti chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama linajumuisha wanachama watano wa kudumu wenye kura ya turufu—China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Amerika—na wengine kumi wa muda, wakiwemo Algeria, Denmark, Ugiriki, Guyana, Pakistan, Panama, Korea Kusini, Sierra Leone, Slovenia, na Somalia