Viongozi wa Magharibi nao wamezea mate kiti cha Oparanya katika ODM
VIONGOZI mbalimbali wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutoka eneo la Magharibi wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kumrithi aliyekuwa Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.
Baadhi ya viongozi hao walio na lengo la kuchukua nafasi ya Bw Oparanya (Naibu Mwenyekiti wa chama hicho) wanatoka katika Kaunti za Kakamega na Vihiga huku wajumbe wa ODM kutoka kaunti hizo mbili wakitaka Fernandes Barasa (Gavana Kakamega) na Godfrey Osotsi (Seneta Vihiga) wamrithi Bw Oparanya.
Mnamo Ijumaa, wajumbe wa ODM kutoka Kaunti ya Kakamega waliidhinisha Bw Barasa kuhudumu kama naibu kiongozi wa chama.
Hii ni baada ya Bw Oparanya kuteuliwa na Rais William Ruto kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya Biashara Ndogo Ndogo.
Bw Oparanya alikuwa akishikilia wadhifa huo pamoja na mwenzake Hassan Joho aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Mombasa kabla ya kuteuliwa katika baraza la mawaziri.
Uteuzi wa Bw Oparanya katika baraza la mawaziri hata hivyo unakabiliwa na changamoto kadhaa baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kudai kwamba gavana huyo wa zamani alijihusisha na shughuli za ufisadi zinazohitaji kuchunguzwa.
Wajumbe wa ODM kutoka Kakamega wakiongozwa na Mbunge wa Lugari (Mbunge) Nabii Nabwera waliteta kwamba kwa kuwa nafasi ya naibu kiongozi wa chama ilikuwa ikishikiliwa na Bw Oparanya kutoka Kaunti ya Kakamega, inafaa wadhifa huo usalie katika kaunti hiyo.